Na George Gabriel

Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, Christopher Magala, amewataka wachimbaji wadogo wa madini katika Kijiji cha Chungu kuzingatia sheria na taratibu za uchimbaji ili kuepuka migogoro na ukiukwaji wa sheria.

Magala alitoa kauli hiyo jana wakati wa ziara yake katika Kijiji cha Chungu, ambapo alikagua shughuli za uchimbaji wa madini na kufuatilia utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa kwa wachimbaji hao.

Alisema wachimbaji wanapaswa kuacha kuvamia maeneo yenye leseni na kuanza uchimbaji bila makubaliano na wenye leseni, akisisitiza kuwa mtu asiye na leseni halali haruhusiwi kufanya shughuli za uchimbaji wa madini kwa mujibu wa sheria.

Aidha, aliwataka wachimbaji kushirikiana na mamlaka husika na kuhakikisha shughuli zao zinafanyika kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.

Magala pia alisisitiza umuhimu wa kudumisha amani na utulivu katika maeneo ya uchimbaji ili kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza kutokana na ukiukwaji wa taratibu.

Kwa upande wao, wachimbaji hao walisema wako tayari kuzingatia sheria na taratibu za uchimbaji wa madini pamoja na kushirikiana na Serikali kuhakikisha shughuli zao zinafanyika kwa utaratibu.

Wakizungumza kwa niaba ya wachimbaji wenzao, Jumanne Mkundapai na Salum Masaga walisema wanapanga kuunda uongozi au kikundi maalumu cha wachimbaji kitakachowasaidia kutambulika rasmi na Serikali.

Walisema chombo hicho kitawawezesha kuwa na uwakilishi wa pamoja wa kuwasilisha changamoto na mahitaji yao kwa Serikali na mamlaka nyingine zinazohusika na shughuli za uchimbaji wa madini.

Aidha, walisema wataendelea kujiepusha na migogoro katika maeneo ya uchimbaji kwa kufuata taratibu na kushirikiana na mamlaka husika.

Waliishukuru Serikali kwa kuwafikia na kusikiliza changamoto zao, wakisema kwa muda mrefu walihisi kutengwa na kukosa nafasi ya kueleza changamoto zinazowakabili katika shughuli zao za uchimbaji wa madini.

Walisema uwepo wa Serikali katika maeneo yao umewapa matumaini na kuwawezesha kupata uelekeo sahihi wa namna ya kufanya shughuli za uchimbaji kwa kuzingatia sheria.

Waliahidi kushirikiana na viongozi na mamlaka husika katika kudumisha amani na utulivu, pamoja na kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinafanyika kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.

Posted in

Leave a comment