
Na Mwandishi Wetu
Zaidi ya watu 30 wanadaiwa kufariki dunia katika ajali mbili tofauti za barabarani zilizotokea usiku wa kuamkia leo, Oktoba 8, 2026, mkoani Morogoro, huku wengine wakijeruhiwa. Miongoni mwa wanaodaiwa kupoteza maisha ni askari wa Jeshi la Polisi waliokuwa kazini.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, ACP Andrew Kantimbo, amethibitisha kutokea kwa ajali hizo na kusema kuwa majeruhi wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.

Amesema idadi kamili ya waliofariki itajulikana baada ya kushirikiana na wataalamu wa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, kutokana na baadhi ya miili kuharibika vibaya baada ya basi kuteketea kwa moto.
Ajali ya kwanza ilitokea eneo la Miti Bora, kati ya Dakawa na Dumila, Wilaya ya Mvomero, majira ya saa 12:45 jioni, Oktoba 8, 2026. Ajali hiyo ilihusisha gari la Polisi lililokuwa na askari waliokuwa kazini na lori aina ya Scania mali ya kampuni ya ATT.
Kwa mujibu wa Kantimbo, watu wanne wamefariki dunia katika ajali hiyo, huku wengine wakijeruhiwa na kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu.
Ajali ya pili ilitokea eneo la Mkambarani, sehemu inayojulikana kama Kikombe cha Chai, Wilaya ya Morogoro, majira ya saa 10:30 usiku wa Oktoba 8, 2026.

Ajali hiyo ilihusisha basi la abiria mali ya kampuni ya Dream Line, lenye namba za usajili T 672 ELT, lililokuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Mbeya, na lori aina ya Scania lenye namba za usajili T 902 ENG, lililokuwa limebeba miti aina ya mirunda na kuelekea Dar es Salaam kutoka Morogoro.
Magari hayo yaligongana uso kwa uso na kuwaka moto, huku basi likiteketea kabisa na kusababisha vifo, majeruhi na uharibifu mkubwa wa magari hayo.
Akizungumzia chanzo cha ajali hiyo, Kantimbo alisema dereva wa lori alijaribu kuyapita magari mengine yaliyokuwa mbele yake bila kuchukua tahadhari katika eneo lisiloruhusiwa.
“Chanzo cha ajali hii ni dereva wa lori kujaribu kuyapita magari mengine yaliyokuwa mbele yake bila kuchukua tahadhari katika maeneo yasiyoruhusiwa,” alisema Kantimbo.
Kamanda huyo amewasihi madereva wa vyombo vya moto kuzingatia sheria na alama za usalama barabarani, akisisitiza kuwa uzembe wa madereva na kupita magari katika maeneo yasiyoruhusiwa kunaweza kusababisha ajali zenye madhara makubwa.
Kwa upande wake, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, Joseph Mwasabeja, alisema jeshi hilo lilifanikiwa kukamilisha zoezi la kuopoa miili ya marehemu na kuwasaidia majeruhi kufikishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu.
Alisema awali walituma gari moja la zimamoto katika eneo la tukio, lakini baada ya kubaini kuwa ajali hiyo ilikuwa kubwa zaidi ya walivyotarajia, waliongeza magari mengine mawili.
“Tulipambana na moto na hatua yetu kubwa ya kwanza ni kuokoa maisha ya watu, na baadaye mali, lakini kulingana na mazingira wakati mwingine mnalazimika kwenda na vyote kwa wakati mmoja,” alisema Mwasabeja.
Alifafanua kuwa katika ajali ya Mkambarani, timu za uokoaji zilifanikiwa kutoa majeruhi 30 na miili 29 ya marehemu hadi majira ya usiku wa manane.
Hata hivyo, alisema idadi hiyo ilikuwa ya awali, akisisitiza kuwa mamlaka za afya ndizo zitakazothibitisha idadi kamili ya waliofariki na kujeruhiwa.
Aidha, alisema jeshi hilo lilituma kikosi kingine katika eneo la Dumila kwa ajili ya operesheni ya uokoaji, ambapo walikuta miili ya watu waliofariki na majeruhi, ambao waliwapeleka hospitalini.

Wakati huo huo, baadhi ya wakazi wa Morogoro, Erica Francis, Asifiwe Honest na Abdul Juma, wameiomba Serikali kuendelea kuboresha miundombinu ya barabara, ikiwemo kuongeza njia katika barabara kuu ya Morogoro–Dar es Salaam.
Walisema hatua hiyo inaweza kusaidia kupunguza ajali za barabarani na kuimarisha usalama wa watumiaji wa barabara.
Hata hivyo, idadi kamili ya vifo pamoja na utambulisho wa watu wote waliofariki bado vinahitaji uthibitisho rasmi kutoka kwa mamlaka husika.

Leave a comment