Na Iddy Mziray, Songea

Jeshi la Polisi Wilaya ya Songea, watumishi wa idara mbalimbali za Serikali na wananchi wamefanya mazoezi ya pamoja kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya polisi na jamii katika kudumisha amani, ulinzi na usalama, pamoja na kutoa elimu ya kujikinga na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño.

Mazoezi hayo yalianzia katika Uwanja wa Zimanimoto, Kata ya Msufini, Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma, na kupita katika kata zaidi ya nne za manispaa hiyo.

Washiriki walifanya matembezi ya kilomita 18 na kuhitimisha kwa kukimbia kilomita tatu, hivyo kutimiza jumla ya kilomita 21.

Mazoezi hayo yaliongozwa na Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Songea, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Juma Balthazar, akishirikiana na Mkuu wa Polisi Jamii wa wilaya hiyo, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Melinda Mgumba.

Akizungumza baada ya mazoezi hayo, ASP Balthazar alisema lengo la shughuli hiyo ni kuimarisha ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi, huku akiwahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda amani na usalama wa nchi.

Alisema hatua hiyo pia inalenga kutoa tahadhari ya mapema na elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kujikinga na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño zinazotarajiwa.

Aidha, aliwataka wananchi kuwa makini na taarifa zinazosambazwa kupitia mitandao ya kijamii, akiwahimiza kutoshawishika na ujumbe unaoweza kuchochea uvunjifu wa amani na kuvuruga usalama wa nchi.

Mazoezi hayo yalifanyika katika hali ya amani na mshikamano, yakionesha ushirikiano kati ya askari polisi na wananchi katika juhudi za kuimarisha ulinzi na usalama wa jamii.

Posted in

Leave a Reply