Na Mwandishi Wetu

Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk. Fidelice Mafumiko, amewataka ndugu wa watu waliofariki katika ajali ya barabarani iliyotokea eneo la Mkambarani, mkoani Morogoro, kufika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kutoa sampuli za vinasaba (DNA) zitakazosaidia kutambua miili ya marehemu.

Ajali hiyo ilihusisha lori aina ya Scania lililokuwa limebeba miti na basi la abiria la kampuni ya Dream Line. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa, watu 32 walifariki dunia na wengine 30 kujeruhiwa baada ya magari hayo kugongana uso kwa uso na moto kuzuka. Moto huo uliteketeza basi na kuharibu baadhi ya miili, hali inayofanya utambuzi wa kawaida kuwa mgumu.

Dk. Mafumiko amesema zoezi la utambuzi linahusisha hatua mbili, ambazo ni kuchunguza miili iliyopatikana na kuchukua sampuli za vinasaba kutoka kwa ndugu wa marehemu. Sampuli hizo zitalinganishwa na matokeo ya uchunguzi wa miili ili kusaidia kuthibitisha utambulisho wa waliofariki.

Amesema Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali itaendelea kushirikiana na uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro pamoja na Mganga Mkuu wa Mkoa kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Best Magoma, amesema hospitali inaendelea kutoa huduma kwa majeruhi waliolazwa kufuatia ajali hiyo.

Posted in

Leave a Reply