Na Furahisha Nundu

Mwenyekiti wa Vyombo vya Habari Kanda ya Kusini mwa Afrika (MISA-TAN), Edwin Soko, amewataka waandishi wa habari kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia misingi ya taaluma yao ili kuhakikisha jamii inapata taarifa sahihi na kwa wakati.

Soko alitoa rai hiyo jana wakati wa mafunzo yaliyowakutanisha waandishi na wahariri wa habari wapatao 60 kutoka Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kati na Kanda ya Magharibi. Mafunzo hayo yalifanyika katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania, jijini Mwanza.

Alisema uandishi wa habari unahitaji umakini, weledi na uzingatiaji wa maadili ya taaluma ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kwa wakati. Aliongeza kuwa, kupitia uandishi wa habari unaozingatia misingi hiyo, vyombo vya habari vinaweza kuchochea uwajibikaji na maendeleo kwa kuibua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii.

Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Mwanza, Daniel Machunda, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa huo, CP Salum Hamduni, alisema jitihada za kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari zinazofanywa na wadau mbalimbali, hususan MISA-TAN, zimekuwa zikichangia kuongeza umakini na kuboresha upatikanaji wa taarifa katika tasnia ya habari.

Machunda alisema Serikali itaendelea kushirikiana na waandishi wa habari kwa kuwapatia taarifa sahihi na kwa wakati ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kuhakikisha wananchi wanapata taarifa kwa wakati muafaka.

Baadhi ya waandishi na wahariri wa habari kutoka vyombo mbalimbali waliohudhuria mafunzo hayo walisema yamekuwa na manufaa katika kuimarisha jitihada za kutoa taarifa kwa jamii. Walisema mafunzo hayo yatawasaidia kuhabarisha umma kuhusu masuala ya maendeleo, amani na demokrasia, pamoja na kuhamasisha mshikamano miongoni mwa wananchi.

Posted in

Leave a Reply