
Na Abel Mwakingwe
Vikundi 21 vya vijana mkoani Rukwa vimepata mikataba ya matengenezo ya barabara yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 285 kupitia Mpango wa Matengenezo ya Kawaida ya Barabara kwa Kutumia Vikundi vya Kijamii (CBRM), unaotekelezwa na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).
Meneja wa TARURA mkoani Rukwa, Mhandisi Chacha Moseti, alisema mikataba hiyo ni sehemu ya Sh milioni 516 zilizotengwa kwa ajili ya vikundi maalumu katika mwaka wa fedha 2026/2027.
Akizungumza katika Maonesho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yanayofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Ndua, Manispaa ya Sumbawanga, alisema kati ya vikundi 38 vinavyoshiriki katika mpango huo mkoani humo, vikundi 21 ni vya vijana, sawa na asilimia 55.
Alisema mpango huo unalenga kuwawezesha vijana kujipatia kipato kupitia kazi za matengenezo ya barabara katika maeneo wanayoishi, huku ukiwahamasisha wananchi kushiriki katika utunzaji wa miundombinu inayowahudumia.
Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi yatakayowawezesha vijana kunufaika na fursa za ajira zinazotokana na shughuli zinazotekelezwa kupitia TARURA.
Kwa upande wake, Msimamizi Msaidizi wa CBRM mkoani Rukwa, Mhandisi Abdulrazak Mshana, alisema mpango huo unawawezesha vijana kupata ajira na kushiriki katika mfumo rasmi wa utoaji wa zabuni.
Alieleza kuwa vikundi hivyo husajiliwa na kushiriki katika taratibu za zabuni kupitia mfumo wa NEST, chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA). Hatua hiyo inaviwezesha vikundi hivyo kutekeleza kazi za matengenezo ya barabara kama wakandarasi katika maeneo yao.
Akizungumzia manufaa ya mpango huo, Mwenyekiti wa kikundi cha Youth Vision Fighters, Florence Clonele, alisema kikundi chake kimepata zabuni ya matengenezo ya barabara ya Pito–Maragano yenye urefu wa kilomita tano.
Naye Mwenyekiti wa kikundi cha Wafugaji Kuku, Justina Malosko, alisema kikundi chake kinahudumia barabara ya Kisiwani–Kichangani yenye urefu wa kilomita tano katika Manispaa ya Sumbawanga.
Viongozi hao wa vikundi walisema mikataba waliyoipata imewasaidia kuongeza kipato, ambacho kinachangia kugharamia mahitaji ya familia zao.
Kupitia mpango wa CBRM, TARURA inalenga kuunganisha matengenezo ya barabara na fursa za kiuchumi kwa jamii, hususan vijana na makundi maalumu, kwa kuwashirikisha moja kwa moja katika utunzaji wa miundombinu katika maeneo yao.


Leave a Reply