
Na Abel Mwakingwe
Serikali kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE), kwa kushirikiana na Vodacom Tanzania Foundation, imeimarisha upatikanaji wa mafunzo ya kitaaluma kwa walimu kwa kutumia teknolojia ya kidijitali, hatua inayolenga kuboresha ufundishaji na kuongeza ubora wa elimu nchini.
Ushirikiano huo unatekelezwa kupitia Programu ya Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini (TCPD/MEWAKA), inayotumia Mfumo wa Usimamizi wa Kujifunza (LMS) pamoja na Vituo vya Rasilimali za Walimu (TRC) kuwawezesha walimu kuendelea kujifunza na kuboresha ujuzi wao.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kituo cha Rasilimali za Walimu katika Shule ya Msingi Naurei, Wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha, Mkuu wa Wilaya hiyo, Neema Lugangira, alisema uwekezaji katika maendeleo ya walimu ni sehemu muhimu ya kuboresha matokeo ya elimu.
Alisema kituo hicho ni cha kwanza kati ya vituo 50 vinavyotarajiwa kujengwa nchini, akieleza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi unaweza kuongeza upatikanaji wa teknolojia na kuweka mazingira bora kwa walimu kujiendeleza kitaaluma.
Lugangira alisema walimu wanapopata maarifa mapya na kutumia teknolojia kwa ufanisi, huongeza uwezo wao wa kuboresha ufundishaji na kuwasaidia wanafunzi kufikia malengo yao ya kitaaluma.
Alibainisha kuwa tathmini ya mahitaji ya programu ya TCPD/MEWAKA, iliyohusisha vituo 178 vya rasilimali za walimu, walimu 350 na wadau mbalimbali, imeonyesha kuwa asilimia 99 ya walimu waliohusishwa wanaifahamu LMS, huku asilimia 71 wakiwa na uelewa wa msingi wa teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA).
Hata hivyo, alisema upatikanaji mdogo wa kompyuta na vifaa vingine vya TEHAMA, huduma za intaneti na usaidizi wa kiufundi bado ni changamoto zinazokwamisha matumizi kamili ya mfumo huo, hasa katika maeneo ya vijijini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Foundation, Zuweina Farah, alisema taasisi hiyo imewekeza katika mifumo na miundombinu inayolenga kuwawezesha walimu kupata mafunzo endelevu na kutumia teknolojia kuboresha taaluma zao.
Farah alisema walimu ni nguzo muhimu katika maendeleo ya elimu, hivyo kuwawezesha kupata maarifa na ujuzi wa kidijitali kunaweza kuwanufaisha wanafunzi na jamii kwa ujumla.
Aliongeza kuwa kupitia ushirikiano na TIE, walimu wanaotumia mtandao wa Vodacom wanaweza kupata maudhui ya mafunzo kupitia mfumo wa LMS bila kutozwa gharama za data, hatua inayolenga kupunguza vikwazo vya upatikanaji wa maudhui hayo.
Alisisitiza kuwa ushiriki wa sekta binafsi katika uwekezaji wa teknolojia, vifaa na utaalamu wa kidijitali ni muhimu katika kujenga mfumo wa elimu unaoendana na mahitaji ya sasa.

Leave a Reply