
Na Mwandishi Wetu
Mawaziri wapatao 26 wanaosimamia masuala ya uchukuzi na lojistiki kutoka nchi wanachama wa Shirika la Bahari la Kanda ya Afrika Mashariki, Kusini na Kaskazini mwa Afrika (MOESNA), wanatarajiwa kukutana jijini Dar es Salaam, Oktoba 15, 2026, kujadili mikakati ya kukuza biashara ya usafiri wa majini na kuimarisha ushiriki wa Afrika katika biashara ya kikanda na kimataifa.
Mkutano huo Mkuu wa 10 wa Baraza la Mawaziri la MOESNA utafanyika katika Hoteli ya Johari Rotana, huku ajenda nyingine muhimu ikiwa ni mpango wa kuanzisha Chuo Kikuu cha Kikanda cha Usafiri kwa Njia ya Maji (RMU), kitakacholenga kuwa kitovu cha elimu, mafunzo, utafiti na ubunifu katika sekta ya usafiri wa majini barani Afrika.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dkt. David Kihenzile, alisema hayo jana alipokuwa akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, kuhusu maandalizi ya mkutano huo.
Alisema Tanzania ipo tayari kushirikiana na nchi wanachama katika hatua za kuanzisha chuo hicho, ambacho kinatarajiwa kuimarisha ujuzi na kuzalisha wataalamu watakaosaidia kukuza sekta ya usafiri wa majini katika ukanda huo.

Alisema chuo hicho kinatarajiwa kuwa Kituo cha Umahiri cha Kikanda kitakachohudumia mahitaji ya nchi wanachama kwa kuimarisha utafiti, ubunifu na mafunzo ya wataalamu wa sekta ya usafiri wa majini.
Alisisitiza kuwa maendeleo ya sekta hiyo hayawezi kutegemea uwekezaji katika bandari, meli na miundombinu pekee, bali yanahitaji pia wataalamu wenye ujuzi, teknolojia na elimu inayokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye.
Katika mkutano huo, mawaziri wanatarajiwa kujadili namna ya kupanua usafirishaji wa mizigo na abiria kwa njia ya meli kati ya bandari za Afrika, pamoja na kuimarisha ushiriki wa kampuni za meli za Afrika katika biashara ya kikanda na kimataifa.
Akizungumzia umuhimu wa sekta hiyo, Dkt. Kihenzile alisema usafiri wa majini ni nguzo muhimu ya maendeleo ya uchumi wa Afrika, akibainisha kuwa zaidi ya asilimia 90 ya biashara ya nje ya bara hilo husafirishwa kwa njia ya bahari.
Aidha, alisema zaidi ya asilimia 80 ya biashara ya bidhaa duniani kwa ujazo husafirishwa kwa njia ya bahari, hali inayosisitiza umuhimu wa kuwa na bandari zenye ufanisi na mifumo bora ya usafirishaji.
Akizungumzia nafasi ya Tanzania katika sekta hiyo, Profesa Mbarawa alisema nchi ina nafasi ya kimkakati katika Bahari ya Hindi na Maziwa Makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa, jambo linaloiwezesha kuwa kiungo muhimu cha biashara kati ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini na masoko ya kimataifa.
Alisema Bandari ya Dar es Salaam huhudumia takribani asilimia 90 ya biashara ya kimataifa ya Tanzania, huku pia ikitoa huduma kwa nchi jirani zikiwemo Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Burundi, Rwanda, Malawi na Uganda.

Aliongeza kuwa shehena iliyohudumiwa katika bandari hiyo iliongezeka kutoka tani milioni 18.41 katika mwaka wa fedha 2021/22 hadi tani milioni 33.75 katika mwaka wa fedha 2025/26, sawa na ongezeko la takribani asilimia 83.
Mkutano huo pia unatarajiwa kuhudhuriwa na wawakilishi wa taasisi za kikanda na kimataifa, zikiwemo Umoja wa Afrika (AU), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Majini (IMO).
Leave a Reply