Na Happy Milion

Wanafunzi watatu wa Shule ya Sekondari Mringa, wilayani Arumeru, mkoani Arusha, wamefariki dunia baada ya kugongwa na lori aina ya Mercedes-Benz katika ajali iliyotokea Oktoba 30, 2026, eneo la Kiushini, Barabara ya Bypass, mkoani humo.

Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Justine Masejo, amesema waliofariki ni Bianka Juma, Catherine Pius na Jesca Sabore, ambao wote walikuwa wanafunzi wa kidato cha tatu.

Kwa mujibu wa Kamanda Masejo, ajali hiyo ilitokea majira ya saa 11 jioni, baada ya lori lenye namba za usajili T.415 DSN, aina ya Mercedes-Benz, lililokuwa limeunganishwa na tela lenye namba T.636 DSG, kuacha njia na kugonga gari dogo aina ya Toyota Rumion lenye namba za usajili T.481 EKZ lililokuwa limeegeshwa kando ya barabara.

Alisema lori hilo lililokuwa likiendeshwa na Abdul Seleman, mkazi wa Arusha, liliwagonga pia wanafunzi hao waliokuwa wakitembea kwa miguu.

Kamanda Masejo alisem chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa lori, ambaye alikuwa akipita magari mengine bila kuchukua tahadhari zinazostahili, hali iliyosababisha kuligonga gari dogo na kushindwa kulidhibiti lori hilo.

Kutokana na tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limewataka madereva wote kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani, kufuata alama za barabarani na kuwa makini na watumiaji wengine wa barabara ili kuepusha ajali zinazoweza kusababisha majeraha na vifo.

Posted in

Leave a Reply