
Na Happy Milion
WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde, ameshuhudia makabidhiano ya mkopo wa Sh bilioni 50 kutoka Benki ya CRDB kwenda kwa kikundi cha wachimbaji wadogo wa dhahabu cha Songwe Gold Family (SGF), kwa ajili ya kuongeza mtaji, kununua mitambo na kuboresha shughuli za uchimbaji.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo, Mavunde amewataka wanachama wa kikundi hicho kutumia mkopo huo kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuongeza uzalishaji na tija katika shughuli zao za uchimbaji.
Amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wachimbaji wadogo kupata mitaji, leseni na taarifa za kijiolojia zitakazowawezesha kuendeleza shughuli zao kwa ufanisi.
Aidha, alisema Serikali itaendelea kuchukua hatua dhidi ya wamiliki wa leseni za uchimbaji ambazo haziendelezwi, ili maeneo hayo yaweze kupewa wachimbaji wenye uwezo na nia ya kuyaendeleza.
Mavunde pia ameipongeza Serikali kwa maelekezo yaliyowezesha maeneo yenye leseni zilizorejeshwa Serikalini kutolewa kwa wachimbaji wadogo, hatua inayolenga kuongeza ushiriki wao katika sekta ya madini.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo amekabidhi leseni za uchimbaji mdogo wa dhahabu kwa vikundi 81 kupitia Mradi wa Mining for a Brighter Tomorrow (MBT), unaolenga kuwawezesha vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kushiriki katika mnyororo wa thamani wa madini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Matawi na Wateja Wadogo na wa Kati wa Benki ya CRDB Tanzania, Bonventure Poul, amesema benki hiyo itaendelea kushirikiana na Wizara ya Madini kuwawezesha wachimbaji wadogo, wachakataji na wafanyabiashara wa madini kupata mitaji kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao.

Poul amesema kati ya mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 426 iliyotolewa na benki hiyo, Sh bilioni 150 zimeelekezwa kwa wachimbaji wadogo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Alhaji Abubakar Kunenge, amesema Serikali itaendelea kuwaunga mkono wachimbaji wadogo kutokana na mchango wao katika kukuza uchumi wa mkoa huo na Taifa kwa ujumla.

Akizungumzia changamoto zinazowakabili wachimbaji, Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Dickson Nickson, amesema upatikanaji wa umeme katika maeneo ya uchimbaji bado ni changamoto, huku akiiomba Serikali kuharakisha hatua za kusambaza nishati hiyo ili kurahisisha shughuli za uzalishaji.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Songwe, Philip Mlugo, ameipongeza Serikali kwa juhudi zake za kuwawezesha wachimbaji wadogo na kuzitaka benki nyingine nchini kuiga mfano wa CRDB kwa kutoa mikopo itakayochochea ukuaji wa sekta ya madini na maendeleo ya kiuchumi.
Leave a Reply