
Na Mwandishi Wetu, Ruvuma
Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma limeendelea kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wananchi na vyombo vya usalama pamoja na matumizi sahihi ya elimu, vipaji na ubunifu wa vijana katika kudumisha amani, mshikamano na maendeleo ya jamii.
Wito huo umetolewa Mei 8, 2026 na Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Ruvuma, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Ramia Mganga wakati wa kikao kazi na Polisi Kata wa mkoa huo kilicholenga kujadili masuala mbalimbali ya kiutendaji na kuweka mikakati ya kuboresha utoaji wa huduma bora kwa wananchi. Kikao hicho kilifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Polisi Mkoa wa Ruvuma.
ACP Mganga aliwataka Polisi Kata kuongeza ushirikiano wa karibu na viongozi wa mitaa, vitongoji, kata pamoja na wananchi ili kusaidia kubaini changamoto mbalimbali zilizopo katika maeneo yao na kuzitatua kwa wakati, hatua itakayosaidia kuhakikisha jamii zinaendelea kuwa salama muda wote.
Aidha, aliwasisitiza kuhakikisha wanafikia makundi yote katika jamii kwa kutoa elimu ya ushirikishwaji wa wananchi katika masuala ya usalama, ili kuongeza uelewa kuhusu madhara ya vitendo vya uhalifu pamoja na umuhimu wa kushirikiana na Jeshi la Polisi. Pia aliwataka kuendelea kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii ili kuimarisha mshikamano kati ya Polisi na wananchi.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Tunduru, Mkaguzi wa Polisi Sonda Mkoyi, amewataka vijana kutumia elimu, vipaji na fani walizonazo kama nyenzo ya kujiletea maendeleo binafsi na ya jamii kwa ujumla.

Akizungumza Mei 8, 2026 wakati wa kongamano la vijana lililofanyika katika Ukumbi wa Skyway wilayani Tunduru, Insp. Mkoyi aliwahimiza vijana kuendelea kuwa mabalozi wa amani, uzalendo na utii wa sheria za nchi, pamoja na kujiepusha na vitendo vya uhalifu, matumizi ya dawa za kulevya, vurugu na ushawishi wa makundi yasiyo na maadili mema.
“Jeshi la Polisi linaamini vijana ni nguvu kazi muhimu ya taifa, hivyo ushirikiano wao katika kudumisha usalama na utulivu wa nchi ni jambo la msingi”, alisema Insp. Mkoyi.
Leave a comment