Na George Gabriel

Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amekipongeza Kikundi cha Vijana Kazi Imara cha Kata ya Nanyumbu, Wilaya ya Nanyumbu, kwa uaminifu katika marejesho ya mikopo, ubunifu na ubora wa bidhaa wanazozalisha.

Kapinga alitoa pongezi hizo jana wakati wa ziara yake wilayani Nanyumbu, ambapo alikagua shughuli mbalimbali zinazofanywa na vijana hao, ikiwemo useremala, ushonaji wa nguo kwa kutumia cherehani pamoja na biashara ya mama ntilie.

Katika ukaguzi huo, Kapinga alivutiwa na ubunifu wa kikundi hicho katika utengenezaji wa vitanda, akieleza kuwa hatua hiyo ni mfano mzuri wa namna vijana wanavyoweza kutumia fursa zinazotolewa na Serikali kuongeza kipato na kujiajiri.

Aidha, alipongeza uaminifu wa kikundi hicho katika kurejesha mkopo wa Shilingi milioni 14.5, ambapo hadi sasa kimefanikiwa kurejesha Shilingi milioni 2.112, hatua aliyosema inaonesha uwajibikaji wa wanakikundi.

Katika kuwatia moyo vijana hao, Kapinga alikabidhi Shilingi milioni moja (TSh 1,000,000), huku akiwataka kuendelea kudumisha uaminifu, kuimarisha ubunifu na kuongeza ubora wa bidhaa zao ili ziweze kushindana katika soko.

Aidha, katika ziara hiyo, Kapinga alitoa mitungi ya gesi kwa wajasiriamali, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama katika shughuli za uzalishaji na matumizi ya kila siku.

Akizungumza na mwandishi baada ya kupokea mtungi wa gesi, Mwajuma Mchakama aliipongeza Serikali kwa kuwajali wananchi na kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi, akisema hatua hiyo itasaidia kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, pamoja na kuboresha mazingira ya kufanyia shughuli zao.

Naye Zamda Ally, mmoja wa wanufaika wa mitungi hiyo ya gesi, aliishukuru Serikali kwa msaada huo, akieleza kuwa ni hatua muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata fursa ya kutumia nishati safi, salama na rafiki kwa mazingira.

Wananchi hao kwa pamoja waliipongeza Serikali kwa kuendelea kusogeza huduma na fursa mbalimbali kwa wananchi, wakisema matumizi ya nishati safi yatasaidia kupunguza athari za matumizi ya nishati zinazoharibu mazingira, pamoja na kuboresha afya na maisha ya familia.

Posted in

Leave a comment