Na Mwandishi Wetu, Songea

Wamiliki wa kampuni za ulinzi mkoani Ruvuma wametakiwa kuhakikisha wanasimamia ipasavyo na kulipa stahiki za askari wao kwa wakati, ili kuwaepusha na vitendo vya uhalifu kama vile wizi wa mali za wananchi pamoja na kuchukua mikopo yenye riba kubwa inayosababisha kukosa uadilifu kazini.

Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Ruvuma, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Ramia B. Mganga, wakati alipokutana na wamiliki, viongozi wa makampuni binafsi pamoja na askari wao katika Bwalo la Polisi Wilaya ya Songea.

ACP Mganga amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wamiliki wa makampuni ya ulinzi, akiwataka kuweka viwango vinavyofanana vya malipo kwa huduma wanazotoa kwa jamii hatua itakayosdaidia kuongeza mapato ya kampuni na hivyo kuwawezesha kuwalipa askari wao vizuri, na kuepuka upungufu wa wafanyakazi unaotokana na malipo duni.

Aidha, amekemea baadhi ya kampuni zinazofanya kazi bila kuzingatia sheria na kanuni za usajili pamoja na umiliki wa silaha akitaja tabia ya kuazimana silaha kuwa ni kinyume cha sheria, na kuwataka kufuata taratibu zote ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria.

Kwa upande wao, askari wa kampuni hizo wameahidi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kuhakikisha usalama katika maeneo yao ya kazi wameonesha utayari wao wa kutoa taarifa za matukio ya uvunjifu wa sheria watakayobaini ili wahusika wachukuliwe hatua stahiki.

Madhumnuni ya mkutano huo yalikuwa ni pamoja na kujadili masuala mbalimbali ya kiutendaji ndani ya kampuni hizo.

Posted in

Leave a comment