Na Mwandishi Wetu, Ruvuma

Wananchi wa Kijiji cha Maposeni wametakiwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za wahalifu na wageni wanaowatia shaka katika maeneo yao ili kudhibiti matukio ya uhalifu.

Kauli hiyo ilitolewa na Polisi Kata wa Maposeni, Mkaguzi wa Polisi (Insp.) Ramadhani Duru, alipokuwa akizungumza na wananchi hao huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano katika masuala ya ulinzi na usalama.

Aidha, aliwataka wananchi kushiriki kikamilifu katika ulinzi shirikishi, kulinda amani na kuepuka vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wa jamii ili kuhakikisha mazingira salama kwa maendeleo ya wananchi.

Katika hatua nyingine, wanafunzi wa Shule ya Msingi Lulimbo, Kata ya Tingi, Tarafa ya Mpepo, Wilaya ya Nyasa, wametakiwa kujiepusha na makundi mabaya yanayoweza kudhoofisha maendeleo yao ya kitaaluma na kuharibu mustakabali wao.

Wito huo ulitolewa jana na Polisi Kata ya Tingi, Mkaguzi wa Polisi (Insp.) Juma Mbwana, alipotembelea shule hiyo kwa ajili ya kutoa elimu kuhusu maadili, usalama na maendeleo ya kijamii kwa wanafunzi.

Aidha, wanafunzi hao walipata ufafanuzi kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia na madhara yake kwa watoto pamoja na jamii. Pia walielekezwa sehemu sahihi za kuripoti matukio ya uhalifu na namna bora ya kutoa taarifa hizo ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa wakati.

Sambamba na hayo, Insp. Mbwana aliwakumbusha madhara ya mimba za utotoni na umuhimu wa kuzingatia maadili mema huku akisisitiza nidhamu shuleni na katika jamii ili waweze kufikia malengo yao ya elimu na maisha kwa ujumla.

Posted in

Leave a comment