
Na Pilastus Nyaulingo
Wataalamu wa teknolojia ya habari na mawasiliano wameitaka Tanzania kuimarisha imani ya wananchi katika huduma za kidijitali, ikiwemo usalama wa mtandao, ulinzi wa taarifa binafsi na ujuzi wa kidijitali, ili nchi iweze kunufaika zaidi na teknolojia ya akili bandia (AI) na uchumi wa kidijitali.
Wito huo umetolewa katika Jukwaa la Tanzania Digital Trust Initiative, lililowakutanisha maofisa wa serikali, wadhibiti, wataalamu wa teknolojia, viongozi wa sekta na wadau wengine kujadili namna ya kujenga mazingira salama na ya kuaminika katika matumizi ya teknolojia nchini.
Akizungumza katika jukwaa hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga, alisema Tanzania imepiga hatua kubwa tangu kupitishwa kwa Sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2003, na kwamba miundombinu iliyojengwa inapaswa kutafsiriwa kuwa manufaa ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi.

Alisema Sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2003 iliweka mkazo katika uanzishaji wa taasisi, miundombinu ya taifa ya TEHAMA na ujuzi wa TEHAMA, huku sera ya mwaka 2016 ikiongeza msisitizo katika mifumo na majukwaa ya kidijitali.
“Tanzania imeingia katika uchumi wa kidijitali na hatua inayofuata ni kujenga miundombinu ya uaminifu itakayowawezesha wananchi kutumia huduma za kidijitali kwa usalama na uhakika,” alisema Dkt. Mwasaga.
Alisema suala la uaminifu ni muhimu zaidi katika biashara za mtandaoni na huduma za kifedha za kidijitali, ambako wananchi wanahitaji kuwa na uhakika kwamba malipo wanayofanya ni salama, taarifa zao binafsi zinalindwa na bidhaa wanazonunua mtandaoni zitawafikia.
“Biashara za mtandaoni zinategemea uaminifu. Bila uaminifu, uchumi wa kidijitali hauwezi kustawi,” alisema Dkt. Mwasaga.
Akizungumzia matumizi ya akili bandia, Dkt. Mwasaga alisema Tanzania haipaswi kutumia teknolojia hiyo kwa kufuata mwenendo wa dunia pekee, bali inapaswa kuangalia namna inavyoweza kutumika kutatua changamoto na kuendana na vipaumbele vya maendeleo ya nchi.
Alitaja sekta za viwanda, kilimo na maendeleo ya uchumi kuwa miongoni mwa maeneo ambayo matumizi sahihi ya AI yanaweza kutoa mchango mkubwa.
Kwa mujibu wa Dkt. Mwasaga, manufaa ya AI yatategemea uwekezaji katika elimu na ujuzi, akitanabaisha kuwa maandalizi duni yanaweza kusababisha teknolojia hiyo kuongeza changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana kutokana na baadhi ya kazi kuchukuliwa na mifumo inayotumia akili bandia.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Privacy Professionals Association (TPPA), Tumwesigye Evans, alisema taasisi hiyo ina jukumu la kulinda taarifa binafsi za watumiaji kadri matumizi ya AI na uchumi wa kidijitali yanavyopanuka.
Alisema TPPA imesaini Mkataba wa Makubaliano (MoU) na Sandbox Security ya India, pamoja na TAFINA, kwa lengo la kuimarisha uaminifu katika huduma za kidijitali nchini.
“Kadri mabadiliko haya yanavyoendelea, ni muhimu kuimarisha imani ya wananchi katika huduma na teknolojia za kidijitali,” alisema Evans.
Alisema ushirikiano huo unalenga kuunganisha ulinzi wa kisheria na hatua za kiufundi na kiusalama ili kulinda watumiaji wa huduma za kidijitali.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kanda wa Mauzo na Masoko wa Sandbox, Amrita Choudhury, alisema ujenzi wa uaminifu katika matumizi ya teknolojia hauwezi kufanywa na taasisi au sekta moja pekee, bali unahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali.
Wadau hao walisema kuimarisha uaminifu wa wananchi katika mazingira ya kidijitali ni muhimu wakati Tanzania ikiendelea kupanua matumizi ya huduma za mtandaoni, biashara za kidijitali na teknolojia mpya kama akili bandia.
Kwa Tanzania, wataalamu wanaamini kuwa kujenga mazingira ya kidijitali yanayoaminika kutasaidia kuongeza matumizi ya huduma za mtandaoni, kulinda watumiaji dhidi ya hatari za kidijitali na kuwezesha teknolojia kuchangia zaidi katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Leave a comment