Na Pilastus Nyaulingo

Tanzania inakabiliwa na changamoto katika kufikia malengo ya kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia, huku gharama za nishati, upatikanaji wa teknolojia na utekelezaji wa sera zikitajwa kuwa miongoni mwa mambo yanayohitaji kupewa kipaumbele.

Wakizungumza kuhusu utekelezaji wa mpango wa Tanzania wa kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia, wadau wa nishati wamesema juhudi zaidi zinahitajika kuhakikisha wananchi wanapata nishati salama, nafuu na inayopatikana kwa urahisi.

Nolasco Mlay kutoka Wizara ya Nishati alisema utekelezaji wa malengo ya nishati safi ya kupikia unahitaji ushirikiano wa Serikali, sekta binafsi, taasisi na wananchi ili kuhakikisha teknolojia hizo zinawafikia watumiaji kwa gharama nafuu.

Alisema Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi yatakayochochea ukuaji wa matumizi ya nishati safi, huku ikilenga kupunguza changamoto zinazowakabili wananchi katika upatikanaji wa uhakika wa nishati hiyo.

Kwa upande wake, Dkt. Prosper Magali wa Tanzania Renewable Energy Association (TAREA) alisema upanuzi wa matumizi ya nishati safi ya kupikia unahitaji kuangalia uwezo wa wananchi kumudu gharama za teknolojia na nishati hizo.

Alisema pamoja na kuwepo kwa teknolojia mbalimbali za nishati safi, wananchi wanahitaji elimu kuhusu faida zake pamoja na mifumo inayowezesha upatikanaji wake kwa gharama nafuu.

Alisema ongezeko la matumizi ya nishati safi ya kupikia linaweza kuwa na manufaa katika maeneo mbalimbali, ikiwemo kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, kulinda mazingira na kupunguza madhara yanayohusishwa na matumizi ya nishati zinazozalisha moshi mwingi.

Hatua hizo zinaweza kuboresha afya za wananchi, hasa wanawake na watoto wanaokaa muda mwingi karibu na maeneo ya kupikia, huku zikisaidia kaya kupunguza muda na gharama za kutafuta kuni au kununua nishati za kupikia.

Kwa Tanzania, matumizi makubwa ya nishati safi yatasaidia kupunguza ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na uzalishaji wa mkaa, hivyo kuchangia uhifadhi wa mazingira.

Hata hivyo, wataalamu wanaeleza kuwa kufikia malengo ya taifa kutahitaji uwekezaji zaidi, ushirikiano wa wadau na kuongeza uelewa wa wananchi ili kuongeza idadi ya kaya zinazotumia nishati salama na nafuu.

Posted in

Leave a comment