Na George Gabriel

Serikali imewataka wataalamu wa tiba asili na tiba mbadala nchini kuendelea kutoa huduma kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyowekwa ili kuhakikisha usalama wa wananchi na kuongeza uaminifu wa huduma hizo katika jamii.

Wito huo umetolewa hivi karibuni na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu, Ibrahim Mwanauta, wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa Wataalamu wa Tiba Asili na Tiba Mbadala uliofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri hiyo.

Mwanauta alisema Serikali inatambua mchango mkubwa wa wataalamu wa tiba asili katika kuboresha huduma za afya, lakini akasisitiza kuwa huduma hizo zinapaswa kutolewa kwa kuzingatia sheria, maadili na weledi wa taaluma hiyo.

“Tiba asili ni sehemu muhimu ya huduma za afya, lakini ni lazima itolewe kwa kuzingatia sheria, maadili na weledi ili kulinda afya za wananchi,” alisema Mwanauta.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu, Dkt. Marco Mazanzagar, aliwataka wataalamu wote kuhakikisha wanajisajili na kupata leseni kutoka Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala kabla ya kuanza kutoa huduma.

Alionya kuwa utoaji wa huduma bila leseni ni kinyume cha sheria na unaweza kuhatarisha afya za wananchi.

Naye Mratibu wa Tiba Asili na Tiba Mbadala Mkoa wa Mtwara, Deogratius Kikota, aliwahamasisha wataalamu kushiriki maadhimisho ya kilele cha Tiba Asili na Tiba Mbadala ngazi ya Mkoa wa Mtwara yatakayofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba mwezi Agosti 2026.

Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Wataalamu wa Tiba Asili Tanzania (BAWATA), Halidi Mohamed Mdoe, aliipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu kwa ushirikiano wake na wataalamu wa tiba asili, akiahidi kuwa chama hicho kitaendelea kuwapatia wanachama wake ushauri, mafunzo na msaada wa kitaalamu ili kuboresha utoaji wa huduma.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa mkutano huo, mtaalamu wa tiba asili Juma Hamisi alisema mafunzo na maelekezo yaliyotolewa yamewaongezea uelewa kuhusu wajibu wa kuzingatia sheria na taratibu za utoaji wa huduma.

“Mkutano huu umetukumbusha wajibu wetu wa kufanya kazi kwa weledi na kufuata sheria. Tutayafanyia kazi maelekezo yote tuliyopewa kwa manufaa ya wananchi,” alisema Hamisi.

Mkutano huo uliwakutanisha wataalamu wa tiba asili na tiba mbadala kutoka maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Nanyumbu kwa lengo la kujadili maendeleo ya sekta hiyo, kuimarisha ushirikiano na Serikali pamoja na kuboresha huduma zinazotolewa kwa jamii.

Posted in

Leave a comment