Na Pilastus Nyaulingo

Kwa mwanafunzi anayekaa darasani siku nzima, kengele ya mwisho inapolia inaweza kumaanisha mwisho wa masomo. Lakini kwa baadhi ya watoto wanaoishi katika maeneo ambayo upatikanaji wa umeme bado ni changamoto, mwisho wa vipindi vya darasani unaweza pia kumaanisha mwisho wa nafasi ya kujisomea kwa siku hiyo.

Hii ni kwa sababu elimu haishii ndani ya darasa. Kuna vitabu vya kusoma baada ya masomo, kazi za kufanya nyumbani, maandalizi ya mitihani na maarifa ya kutafuta nje ya muda rasmi wa vipindi. Bila mwanga wa kutosha, muda huo unaweza kupotea.

Katika Tanzania, mjadala kuhusu upatikanaji wa nishati umeendelea kuhusishwa na upatikanaji wa huduma muhimu, ikiwemo elimu.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Benki ya Dunia imeonesha namna upatikanaji wa umeme unavyoweza kuboresha mazingira ya kujifunza, matumizi ya teknolojia na huduma nyingine shuleni.

Muda wa Kusoma Haupaswi Kuishia Jua Linapozama

Kwa mwanafunzi wa shule ya sekondari, muda wa kujisomea baada ya vipindi unaweza kuwa muhimu katika kuelewa masomo, kufanya kazi za shule au kujiandaa kwa mitihani.

Lakini pale ambapo shule au mazingira ya nyumbani hayana umeme wa uhakika, mwanafunzi anaweza kulazimika kusoma kwa mwanga hafifu au kuacha kabisa kusoma wakati wa usiku.

Uzoefu wa Shule ya Sekondari Lukaranga unaonyesha tofauti ambayo umeme unaweza kuleta katika mazingira ya elimu.

Baada ya shule hiyo kupata umeme, wanafunzi waliweza kutumia muda wa jioni kujisomea katika mazingira yenye mwanga na usalama zaidi.

Japhet Tobeka, aliyekuwa mwanafunzi wa Kidato cha Nne wakati huo, anaeleza namna upatikanaji wa umeme ulivyowapa wanafunzi nafasi ya kurudi shuleni jioni na kuendelea na masomo katika mazingira bora zaidi.

Kauli hiyo inaonyesha kuwa umeme si suala la kuwasha taa pekee. Ni miundombinu inayoweza kuongeza muda ambao mwanafunzi anaweza kutumia kujifunza.

Kwa mtoto wa kike, muda huo unaweza kuwa na umuhimu zaidi, hasa katika mazingira ambayo majukumu ya nyumbani au changamoto nyingine zinaweza kupunguza muda wake wa kusoma.

Kwa Nini Suala Hili Ni Muhimu Zaidi kwa Wasichana?

Wasichana wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazoweza kuathiri mwendelezo wa elimu, hasa wanapofikia umri wa balehe.

Kwa mujibu wa ripoti za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto ( UNICEF Tanzania) zinaeleza kuwa mamilioni ya watoto wenye umri wa kwenda shule hawapo shuleni, huku wasichana kutoka maeneo ya vijijini na kaya maskini wakiwa miongoni mwa wanaoweza kukabiliwa zaidi na vikwazo vya kuendelea na elimu.

Changamoto hizo zinaweza kuhusisha umaskini, huduma duni za maji na usafi, changamoto wakati wa hedhi pamoja na ndoa za utotoni.

Hivyo, tunapozungumzia umeme shuleni, hatupaswi kuutazama kama suala linalojitegemea. Ni sehemu ya mazingira mapana yanayoweza kumsaidia mtoto wa kike kubaki shuleni, kujifunza kwa ufanisi na kutumia muda wake vizuri.

Shule yenye mwanga wa kutosha inaweza pia kuwa mazingira salama zaidi kwa wanafunzi wanaohitaji kubaki shuleni baada ya muda wa kawaida wa masomo.

Umeme Unabadilisha Zaidi ya Taa

Faida ya umeme shuleni haiishii kwenye kusoma vitabu usiku.

Umeme unaweza kuwezesha matumizi ya kompyuta, vifaa vya kidijitali, uchapishaji wa vifaa vya kujifunzia na matumizi ya teknolojia nyingine zinazohitaji nishati.

Hili linaonekana pia katika uzoefu wa Shule ya Sekondari Lukaranga.

Kabla ya shule hiyo kupata umeme, walimu walikabiliwa na changamoto katika kupata na kuandaa baadhi ya vifaa vya kufundishia. Baada ya umeme kupatikana, mazingira ya kazi yalibadilika na matumizi ya vifaa vya kielektroniki yakawa rahisi zaidi.

Mwalimu Flora Chacha anaeleza kuwa kabla ya shule kupata umeme, changamoto ya upatikanaji wa vifaa vya kuchapisha iliwalazimu wakati mwingine kwenda maeneo mengine kupata huduma hiyo. Baada ya shule kuunganishwa na umeme, walimu waliweza kuchapisha nakala za vitabu na kutumia vifaa vya sauti katika ufundishaji.

Mabadiliko hayo yanaonyesha uhusiano uliopo kati ya nishati na ubora wa elimu. Kadiri shule inavyokuwa na uwezo wa kutumia teknolojia, ndivyo inavyoweza kupanua njia ambazo mwanafunzi anajifunza.

Kwa mtoto wa kike, ambaye tayari anaweza kukutana na vikwazo vingine vya kijamii na kiuchumi, mazingira bora ya kujifunza yanaweza kuwa na umuhimu mkubwa katika kuendelea na masomo.

Umeme Unamsaidia Pia Mwalimu

Mjadala wa umeme na elimu wakati mwingine huangalia zaidi upande wa mwanafunzi, lakini mwalimu naye anahitaji mazingira yanayomwezesha kufanya kazi yake vizuri.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Lukaranga, Joseph Tongora, anasema kabla ya shule kupata umeme walikabiliwa na changamoto katika kufanya tathmini za mara kwa mara, jambo lililoathiri namna walivyoweza kufuatilia maendeleo ya wanafunzi.

Baada ya shule kupata umeme, walimu waliweza kufanya tathmini za kila wiki kwa urahisi zaidi.

Hili ni muhimu kwa sababu ubora wa elimu hauamuliwi na mwanafunzi pekee. Mwalimu anahitaji vifaa, muda na mazingira yanayomwezesha kutambua changamoto za mwanafunzi na kumsaidia kwa wakati.

Kwa hiyo, umeme unapowezesha mwalimu kuandaa vifaa, kufanya tathmini na kutumia teknolojia, athari yake inaweza kufika hadi kwa mwanafunzi.

Kutoka Mwanga Hadi Fursa

Tanzania imepiga hatua katika kuongeza upatikanaji wa umeme. Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, upatikanaji wa umeme nchini uliongezeka kutoka asilimia 14 mwaka 2011 hadi asilimia 46 mwaka 2022.

Hata hivyo, tofauti kati ya maeneo ya mijini na vijijini bado ilikuwa kubwa, huku upatikanaji ukiwa asilimia 73.2 mijini ikilinganishwa na asilimia 24.5 vijijini.

Takwimu hizi zinaonyesha kwa nini mjadala wa umeme na elimu hauwezi kutenganishwa na mjadala wa maendeleo ya vijijini.

Iwapo shule ya kijijini haina umeme, wanafunzi wake wanaweza kukosa baadhi ya fursa ambazo wanafunzi wa shule zilizounganishwa kwenye umeme wanazipata na hiyo ikwa ni sababu mojawapo kuwatofatisha na wengine wenye huduma ya umeme.

Tofauti hiyo inaweza kuonekana katika matumizi ya teknolojia, muda wa kujisomea na uwezo wa walimu kutumia vifaa mbalimbali vya kufundishia.

Ndiyo maana uwekezaji katika nishati unaweza pia kuonekana kama uwekezaji katika usawa wa elimu.

Changamoto Bado Haijaisha

Pamoja na maendeleo yaliyopatikana, upatikanaji wa umeme pekee hauwezi kutatua changamoto zote za elimu.

Shule inahitaji walimu wenye ujuzi, vifaa vya kujifunzia, madarasa salama, maji, vyoo vinavyofaa, vitabu na mazingira yanayomruhusu mwanafunzi kujifunza kwa utulivu.

Lakini pia ni muhimu kutambua kwamba miundombinu moja inaweza kuwezesha nyingine kufanya kazi vizuri zaidi.

Kompyuta haiwezi kutumika bila umeme. Vifaa vya kuchapisha haviwezi kufanya kazi bila nishati. Mwanafunzi hawezi kutumia baadhi ya teknolojia za kujifunzia bila chanzo cha umeme.

Kwa hiyo, nishati ni sehemu ya msingi ya mazingira ya kisasa ya elimu.

Swali si Kama Tunaweka Umeme Pekee

Tunapofikiria kuhusu elimu ya mtoto wa kike, mara nyingi tunazungumzia ada, sare, vitabu na walimu. Hayo yote ni muhimu.

Lakini mazingira yanayomzunguka mtoto pia yanaamua kwa kiwango fulani kama ataweza kutumia fursa hiyo ya elimu kikamilifu.

Umeme unaweza kuonekana kama kitu kidogo unapoutazama kama taa inayowaka ukutani. Lakini kwa mwanafunzi anayehitaji saa moja zaidi ya kujisomea, kwa mwalimu anayehitaji kuandaa vifaa vya somo au kwa shule inayotaka kutumia teknolojia, mwanga huo unaweza kumaanisha mengi zaidi.

Uzoefu wa Shule ya Sekondari Lukaranga unaonyesha kuwa mabadiliko hayo yanaweza kuonekana katika maisha ya kila siku ya shule, kuanzia muda wa wanafunzi kujisomea hadi uwezo wa walimu kuandaa vifaa na kufanya tathmini.

Hatimaye, kuhakikisha shule zina nishati ya uhakika si suala la kuongeza mwanga kwenye majengo pekee. Ni kuongeza muda wa kujifunza, uwezo wa kutumia teknolojia na mazingira yanayoweza kumsaidia mtoto kufikia ndoto zake.

Kwa mtoto wa kike anayekua katika mazingira yenye changamoto, wakati mwingine tofauti kati ya kuendelea na safari ya elimu na kukata tamaa inaweza kuanza na jambo rahisi kama kupata mazingira salama na yenye mwanga wa kujifunzia.

Posted in

Leave a comment