Na Alex Msumeno

Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo nchini, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Simon Pasua, amewataka viongozi wa kimila kuwa wasuluhishi wa migogoro katika jamii zao na kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuzuia migogoro baina ya wakulima na wafugaji.

Wito huo umetolewa leo katika mnada wa mifugo uliopo Kata ya Kwala, Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani, ambapo SACP Pasua alisema viongozi wa kimila katika jamii za wakulima na wafugaji wanapaswa kushirikiana na viongozi wa Serikali katika kutatua migogoro inayojitokeza.

Alisema viongozi hao wanapaswa kutoa maelekezo kwa vijana wao, ikiwemo kutafuta maeneo ya malisho, mazizi na mabwawa ya maji yaliyo mbali na mashamba ya wakulima, ili kuepusha migogoro ambayo inaweza kusababisha mapigano na malumbano.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wafugaji wa Kata hiyo, Mzee Kieleni, alimshukuru Kamanda Pasua kwa kutembelea mnada huo na kusema huduma zinazotolewa na Jeshi la Polisi zimekuwa na mchango mkubwa katika kupunguza uhalifu na kuwabaini wahalifu, hususan kupitia Polisi Kata wanaoshirikiana na wananchi.

Alisema pamoja na elimu waliyopata kuhusu namna ya kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu, wameelimishwa pia kuhusu ujenzi wa mazizi salama na njia za kutatua migogoro inayojitokeza katika shughuli zao za ufugaji.

Aidha, aliomba Serikali itenge maeneo maalumu kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji ili kuepusha migogoro inayojitokeza mara kwa mara baina ya wakulima na wafugaji.

Posted in

Leave a comment