Waziri Saidi, Tabora

Mkuu wa Polisi Jamii wa Tabora Manispaa, SP Honorata Oisso, amewaongoza maafisa na wakaguzi wa Jeshi la Polisi katika hafla ya kumuaga na kumpongeza Mkaguzi Mstaafu Hassara Mkobela.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Tabora Manispaa jana katika Bwalo la Polisi, SP Novatus Nyabenda, ambaye pia ni Mkuu wa Usalama Barabarani wa Tabora Manispaa, SP Oisso alimpongeza kwa utumishi wake na mchango wake katika Jeshi la Polisi.

Aidha, alizungumzia umuhimu wa mshikamano, ushirikiano na matendo ya huruma miongoni mwa askari, akieleza kuwa matendo hayo yanapaswa kuanzia ndani ya Jeshi la Polisi kabla ya kuifikia jamii.

Alisema mshikamano na ushirikiano mzuri miongoni mwa askari ni sehemu muhimu ya kujenga uhusiano mzuri na jamii, jambo litakalosaidia katika kuzuia na kupunguza uhalifu pamoja na wahalifu katika Manispaa ya Tabora.

Kwa upande wake, Happiness Mwakipesile, ambaye ni mtoto wa Mkaguzi mstaafu, aliwashukuru maafisa na askari wa Jeshi la Polisi kwa kuandaa hafla hiyo na kuendelea kudumisha ushirikiano mzuri.

Alisema ushirikiano huo unatoa taswira nzuri kwa jamii na familia kwa ujumla, huku akieleza kuwa hafla hiyo imemfundisha mambo mengi kuhusu mshikamano na upendo miongoni mwa askari.

“Ushirikiano huu ni mzuri na unaleta picha nzuri kwa jamii na familia kwa ujumla. Leo nimejifunza mambo mengi,” alisema Happiness.

Katika hafla hiyo, askari walipata fursa ya kula pamoja, kupiga picha za pamoja na kumpatia Mkaguzi Mstaafu Hassara Mkobela zawadi mbalimbali kama ishara ya kumpongeza na kumtakia heri katika hatua yake mpya ya maisha.

Posted in

Leave a comment