Na George Gabriel

Wananchi wa Kijiji cha Mkuula, Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara, wameeleza kufurahishwa na mpango wa ujenzi wa mnara wa redio wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), wakisema mradi huo utawasaidia kupata taarifa mbalimbali za kitaifa na kijamii pamoja na burudani kwa wakati.

TBC, kwa kushirikiana na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), inatarajia kuanza ujenzi wa mnara huo katika Kijiji cha Mkuula, hatua inayolenga kuboresha usikivu wa matangazo ya TBC Taifa na Bongo FM katika maeneo ya Wilaya ya Nanyumbu.

Akizungumza katika mkutano wa kijiji uliofanyika Agosti 13, 2026, Mkuula, Bi. Faith Munyi kutoka UCSAF alisema maandalizi ya ujenzi wa mnara huo tayari yameanza kwa hatua za awali.

Alisema ujenzi huo unatarajiwa kutekelezwa kwa kasi ili kuhakikisha wananchi wa Wilaya ya Nanyumbu wanapata huduma bora ya redio kwa wakati, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wananchi katika kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa mafanikio.

Katika mkutano huo, wananchi wa Kijiji cha Mkuula walionyesha utayari wa kushirikiana na utekelezaji wa mradi huo kwa kutoa eneo la ujenzi wa mnara bila malipo.

Wananchi hao wameeleza matumaini kuwa uwepo wa mnara huo utachangia maendeleo ya kijiji kwa kuimarisha upatikanaji wa taarifa muhimu, elimu na burudani kwa jamii.

Akizungumza na mwandishi wa habari, Mzee Juma Payao alisema wananchi wamefurahishwa sana na ujio wa mradi huo, huku akiishukuru TBC pamoja na Serikali kwa kuwakumbuka na kuwaletea huduma hiyo.

Alisema kwa muda mrefu wananchi wa Mkuula wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kutopata matangazo ya redio kwa urahisi, hali iliyowafanya kukosa taarifa mbalimbali muhimu zinazotolewa kupitia vyombo vya habari.

“Tunashukuru sana TBC na Serikali kwa ujumla kwa kutuletea mradi huu. Tunaamini mnara huu utatusaidia kupata taarifa na burudani kwa wakati,” alisema Mzee Payao.

Kwa upande wake, Zuhula Khalifani alieleza furaha yake kwa ujio wa mradi huo, akisema utakuwa mkombozi kwa wananchi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikosa taarifa kutokana na changamoto ya usikivu wa redio.

Alisema upatikanaji wa taarifa kupitia redio utawasaidia wananchi kufahamu mambo mbalimbali yanayoendelea ndani na nje ya eneo lao, pamoja na kupata elimu na burudani.

Ujenzi wa mnara huo unatarajiwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za utangazaji kwa wananchi wa Nanyumbu, hususan katika maeneo ambayo yamekuwa yakikabiliwa na changamoto ya usikivu wa redio.

Posted in

Leave a comment