Na Jastini Bukebuke, Geita

Mkaguzi wa Polisi Kata ya Nyakafulu, INSP Denis Rwehumbiza, amewataka wanafunzi kutovumilia wala kuficha vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa nyumbani au shuleni, badala yake watoe taarifa kwa walimu, wazazi, viongozi wa maeneo yao au Jeshi la Polisi ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahusika.

Rai hiyo ameitoa leo alipokuwa akitoa elimu kuhusu kinga dhidi ya ukatili kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Ilolangulu, iliyopo Kata ya Ilolangulu, Wilaya ya Mbogwe, mkoani Geita.

INSP Rwehumbiza aliwataka wanafunzi kuwa waangalifu dhidi ya vishawishi kutoka kwa watu wasiowafahamu, ikiwemo kupokea zawadi kama pipi, chipsi, fedha au msaada wa usafiri (lifti), akieleza kuwa mazingira hayo yanaweza kutumika kuwarubuni na hatimaye kuwaingiza katika vitendo vinavyohatarisha maisha na mustakabali wao.

Alisema baadhi ya madhara yanayoweza kujitokeza ni pamoja na kuacha shule, kupata mimba za utotoni na kujiingiza katika mazingira hatarishi yanayoweza kuathiri maendeleo yao.

Kwa upande wake, Mwalimu wa Nidhamu wa Shule ya Sekondari Ilolangulu, Fanuel Wilfred, aliwahimiza wanafunzi kuwa mstari wa mbele kutoa taarifa kuhusu watu wanaowadanganya au kuwarubuni ili hatua za kisheria zichukuliwe mapema.

Alisema ushirikiano kati ya wanafunzi, walimu, wazazi na vyombo vya dola ni muhimu katika kuzuia vitendo vya ukatili na kuhakikisha mazingira salama ya kujifunzia.

Elimu hiyo imelenga kuongeza uelewa wa wanafunzi kuhusu namna ya kujilinda dhidi ya ukatili na unyanyasaji, pamoja na kuwajengea ujasiri wa kutoa taarifa kwa mamlaka husika wanapokumbana na vitendo hivyo.

Akihitimisha, INSP Rwehumbiza aliwahimiza wanafunzi kusoma kwa bidii, kuzingatia nidhamu na kujituma ili kutimiza ndoto zao za kielimu na kujenga maisha yenye mafanikio.

Posted in

Leave a comment