Na George Gabriel

Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, Christopher Edward Magala, amefungua rasmi mafunzo ya awali ya Jeshi la Akiba kwa mwaka 2026 yanayofanyika katika Kata ya Likokona, yakilenga kuwajengea washiriki uzalendo, nidhamu na ujuzi wa msingi wa ulinzi na usalama wa Taifa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo uliofanyika Julai 13, 2026, katika viwanja vya Shule ya Msingi Likokona B, Magala alisema Jeshi la Akiba lina nafasi muhimu katika kuimarisha usalama wa nchi na kujenga uzalendo miongoni mwa wananchi. Aliwataka washiriki kuyatumia vyema mafunzo hayo na kuwa tayari kulitumikia Taifa watakapohitajika.

Jumla ya washiriki 82 wamejiunga na mafunzo hayo, wakiwemo wanaume 73 na wanawake 9. Washiriki hao wanatarajiwa kupata mafunzo ya msingi ya kinadharia na vitendo yatakayowawezesha kutekeleza majukumu ya Jeshi la Akiba kwa ufanisi.

Mmoja wa washiriki, Said Mtailika, alisema ameridhishwa na uamuzi wa Serikali kuendelea kutoa mafunzo ya Jeshi la Akiba kwa wananchi, akieleza kuwa yatamjengea uwezo wa kujitambua, kuimarisha nidhamu na kuongeza uzalendo.

Aliwahimiza vijana wengine kutumia fursa hiyo badala ya kuipuuzia, akisema mafunzo hayo yana manufaa makubwa kwa maendeleo yao binafsi na kwa Taifa kwa ujumla.

Naye mzazi Kalanje Abdarah aliwashukuru viongozi wa Serikali kwa kuanzisha mafunzo hayo wilayani Nanyumbu, akisema yatasaidia kuwajenga vijana katika maadili mema, nidhamu na kuwajibika kwa jamii.

Aidha, aliwasihi washiriki wote kutokukata tamaa au kukimbia mafunzo kutokana na changamoto zinazoweza kujitokeza, bali wavumilie hadi watakapohitimu, kwani maarifa na stadi watakazopata yatakuwa msingi muhimu katika maisha yao ya baadaye.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuendelea kwa kipindi kilichopangwa, huku washiriki wakipatiwa mafunzo mbalimbali ya kinadharia na vitendo yatakayowawezesha kutekeleza majukumu ya Jeshi la Akiba kwa weledi, nidhamu na uzalendo.

Posted in

Leave a comment