
Na Jastini Bukebuke
Madereva wa bodaboda na bajaji za mizigo katika Mtaa wa Shinyanga A, Kata ya Nyakafulu, Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita, wamepatiwa elimu kuhusu umuhimu wa ulinzi shirikishi na malezi bora ya watoto, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha usalama na ustawi wa jamii.
Akitoa elimu hiyo juzi, Staff Sajenti (SSGT) wa Jeshi la Polisi, Mohamed Bujiku, aliwataka madereva hao kuacha tabia ya kufumbia macho vitendo vya uhalifu, akieleza kuwa baadhi ya wahalifu hutegemea ushirikiano wa madereva kusafirisha watuhumiwa, mali za wizi au mizigo inayohusishwa na vitendo vya kihalifu.

Alisisitiza kuwa ushiriki wa madereva katika kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kuhusu watu au matukio yanayotiliwa shaka ni hatua muhimu ya kuzuia uhalifu na kulinda amani, usalama wa wananchi pamoja na mali zao.
Aidha, aliwahimiza kushiriki kikamilifu katika shughuli za ulinzi shirikishi, akieleza kuwa mfumo huo ni nguzo muhimu ya kudumisha usalama, kuimarisha ushirikiano kati ya wananchi na Jeshi la Polisi, na kujenga jamii yenye amani, mshikamano na uwajibikaji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kijiwe hicho, Amon Kidenya, aliwataka madereva hao kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za usafirishaji barabarani ili kuepuka ajali.
Pia alisisitiza kuwa malezi bora ya watoto ni jukumu la kila mwanajamii, akieleza kuwa ushirikiano wa wananchi katika kuhakikisha watoto wanalelewa katika maadili mema unachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza vitendo vya uhalifu na kujenga kizazi chenye nidhamu, uzalendo na uwajibikaji.

Leave a comment