Na Damasi Kalembwe

Kikosi cha Usalama Barabarani kwa kushirikiana na uongozi wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (UDART) kilifanya kikao kazi na madereva wa mabasi ya mwendokasi katika ukumbi wa Chuo cha Teknolojia cha Dar es salaam (DIT) ili ,  kujadili na kuweka mikakati ya kupunguza ajali zinazotokea katika mfumo wa usafiri wa mabasi yaendayo haraka.

Katika kikao hicho, ilielezwa kuwa kati ya asilimia 65 na 70 ya ajali zinazohusisha mabasi ya mwendokasi husababishwa na makosa ya kibinadamu, ikiwemo ulevi, uzembe na mwendo kasi usiozingatia sheria huku asilimia zilizobaki ni ajali kutokana na changamoto za miundombinu pamoja na hitilafu za kiufundi katika baadhi ya magari.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Kinondoni, SSP Adamson Mwangamilo, alisisema ni muhimu kufunga viashiria vya mwanga kwenye vizuizi barabarani ili kuongeza usalama, huku akiwahimiza wananchi kutumia daraja la juu la waenda kwa miguu eneo la Kimara Mwisho badala ya kuvuka barabara kiholela, hatua itakayosaidia kupunguza ajali na msongamano wa magari.

Kwa upande wake, Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Ilala (RTO), SSP Salum M. Morimori, alionya kuwa vitendo vya uzembe, ulevi wakati wa kuendesha, pamoja na kukaidi taa na alama za usalama barabarani havitavumiliwa.

Aliwataka madereva kuzingatia kanuni za udereva wa kujihami ili kupunguza ajali, hususan katika maeneo yenye msongamano mkubwa kama Kivukoni na Msimbazi.

Naye Mkurugenzi wa UDART, Pius Ng’ingo, aliahidi kushughulikia changamoto za kiufundi zinazohusu mabasi ya mwendokasi na kuimarisha usimamizi wa nidhamu kwa madereva na watumishi wote ili kuongeza usalama wa huduma zinazotolewa.

Akizungumza kwa niaba ya madereva, Nassoro Hoza aliahidi ushirikiano wa karibu na Jeshi la Polisi pamoja na uongozi wa UDART katika kutekeleza kaulimbiu ya “Utii wa Sheria Bila Shuruti”, akisema madereva watazingatia udereva wa kujihami ili kulinda maisha ya abiria, watumiaji wengine wa barabara na vyombo vya usafiri wanavyoviendesha.

Kikao hicho ni sehemu ya juhudi zinazoendelea za Jeshi la Polisi na UDART za kuimarisha usalama barabarani, kupunguza ajali na kuhakikisha huduma za usafiri wa mabasi ya mwendokasi zinaendelea kutolewa kwa usalama na ufanisi.

Posted in

Leave a comment