

Na Damasi Kalembwe
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni, kupitia Kitengo cha Ushirikishwaji wa Jamii, limetoa msaada wa mahitaji mbalimbali kwa vituo vya kulelea watoto wenye mahitaji maalumu vya New Life na Huruma Children Home, vilivyopo Wilaya ya Kinondoni, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha ustawi wa watoto hao na kudumisha mahusiano mema kati ya Jeshi la Polisi na jamii.
Mkuu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Jamii Mkoa wa Kinondoni, ACP Ally Shughuli Wendo, aliyemwakilisha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, SACP Mtatiro Kitinkwi, aliongoza ziara hiyo akiwa ameambatana na maafisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali.
Katika ziara hiyo, Jeshi la Polisi lilikabidhi msaada uliojumuisha unga, mchele, sukari, mafuta ya kula, taulo za kike, pampasi na mahitaji mengine muhimu kwa ajili ya kusaidia malezi na ustawi wa watoto wanaolelewa katika vituo hivyo.
Akizungumza kwa niaba ya watoto wanaolelewa katika vituo hivyo, Abdul Issa alilishukuru Jeshi la Polisi kwa msaada huo, akieleza kuwa umewaletea faraja na matumaini, huku ukidhihirisha moyo wa kujitolea na kuwajali watoto wenye mahitaji maalumu.
Alisema mchango huo una umuhimu mkubwa katika kuboresha mazingira ya malezi na kukidhi baadhi ya mahitaji muhimu ya kila siku ya watoto hao.
Ziara hiyo ni sehemu ya shughuli za ushirikishwaji wa jamii zinazotekelezwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni, zenye lengo la kuimarisha uhusiano kati ya Polisi na wananchi, pamoja na kuhamasisha jamii kushiriki katika kuwasaidia watoto na makundi mengine yenye mahitaji maalumu.
Leave a comment