
Na Damasi Kalembwe
Jeshi la Polisi, kupitia Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Kinondoni, SP Edna Maro, limetoa elimu ya usalama kwa wafanyakazi wa Hoteli ya Golden Tulip iliyopo Masaki, Dar es Salaam, likiwataka kutambua kuwa kila mmoja ana wajibu wa kulinda mali za hoteli na kutekeleza majukumu yake kwa weledi huku akiepuka kujihusisha na vitendo vya uhalifu vinavyoweza kuharibu taswira ya hoteli na nchi kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, SP Maro alisema wizi ni kosa la jinai na kuwahimiza wafanyakazi kutoa taarifa kwa uongozi wa hoteli pamoja na Jeshi la Polisi wanapobaini viashiria vya uhalifu.

Aidha, aliwataka kuwa walinzi wa wenzao, kuwapokea wageni na viongozi kwa heshima, kudumisha umoja mahali pa kazi na kufahamu adhabu zinazotokana na makosa ya wizi kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande wake, Mkaguzi wa Polisi wa Kata ya Msasani, Mkaguzi Joel Kaaya, aliwakumbusha umuhimu wa huduma bora kwa wateja wanaoingia na kutoka hotelini kwa kuwa huchangia kuimarisha usalama, kuongeza imani ya wageni na kukuza sekta ya utalii nchini.

Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa hoteli, Bi. Grace Karsan alilishukuru Jeshi la Polisi kwa kutoa mafunzo hayo, akisema yameongeza uelewa wa wafanyakazi kuhusu masuala ya usalama.
Naye Miraji Juma, akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi, aliomba mafunzo kama hayo yaendelee kutolewa mara kwa mara katika hoteli mbalimbali ili kuongeza uelewa wa masuala ya usalama na kuwajengea wafanyakazi uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Leave a comment