Na Farida Mkumba, Dodoma

Wananchi wa vijijini wanatarajiwa kuanza kunufaika na mfumo mpya wa mita za maji za malipo kabla (prepaid), unaolenga kuondoa kero ya bili kubwa za maji na kuwapa watumiaji uhuru wa kutumia maji kulingana na kiasi cha fedha walicholipia.

Akizungumza wakati wa Maonesho ya Nane Nane yaliyofanyika katika Viwanja vya John Samuel Malecela, Nzuguni, jijini Dodoma, Afisa Habari na Masoko wa RUWASA, Haji Athumani Msovu, alisema mfumo huo unafanya kazi kwa utaratibu unaofanana na mita za umeme za LUKU, ambapo mtumiaji hulipia huduma ya maji kabla kwa kiasi anachokihitaji.

Alisema teknolojia hiyo italeta uwazi zaidi katika utoaji wa huduma za maji, kwani kila mtumiaji atatumia maji kulingana na kiasi cha fedha alicholipa, hivyo kuondoa malalamiko yanayotokana na bili zisizoeleweka.

Msovu alisema uwekaji wa mita hizo tayari umeanza katika baadhi ya Vyombo vya Usimamizi wa Huduma za Maji vya Kijamii (CBWSO) katika mikoa mbalimbali, na kwamba mrejesho wa awali kutoka kwa wananchi umeonyesha kuridhishwa na mfumo huo.

Alieleza kuwa RUWASA imesaini mkataba na Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) kwa ajili ya kutengeneza mita hizo hapa nchini. Baada ya majaribio yaliyofanyika, alisema mita zilizotengenezwa na ATC zimeonyesha ufanisi mkubwa na tayari zimeanza kusambazwa katika baadhi ya mikoa inayohudumiwa na RUWASA.

Kwa mujibu wa Msovu, ushirikiano huo utawezesha CBWSO na Mamlaka za Maji kununua mita hizo moja kwa moja kutoka ATC kulingana na bajeti na mahitaji yao, hatua itakayorahisisha upatikanaji wa vifaa hivyo.

Aidha, alisema mita hizo zimetengenezwa kwa plastiki maalumu isiyoshambuliwa na kutu, jambo linalozifanya zifae hata katika maeneo yenye maji yenye kiwango kikubwa cha chumvi. Aliongeza kuwa teknolojia hiyo itasaidia kupunguza uharibifu wa mita na gharama za matengenezo.

Msovu alisema RUWASA itaendelea kupokea maoni kutoka kwa wananchi ili kuboresha zaidi mfumo huo na kuhakikisha unatoa huduma bora na yenye ufanisi katika maeneo yote utakakotekelezwa nchini.

Posted in

Leave a comment