Na Mwandishi Wetu, Nachingwea—Lindi

Mbunge wa Jimbo la Nachingwea, Fadhili Liwaka, amekabidhi gari la kubebea wagonjwa (ambulance) katika Kituo cha Afya Naipanga, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa jimbo hilo.

Makabidhiano hayo yamefanyika wakati Mbunge huyo akiendelea na ziara yake ya kuwashukuru wananchi kwa imani waliyoonyesha kwake, sambamba na kusikiliza changamoto na kero mbalimbali zinazowakabili.

Mbali na kukabidhi ambulance hiyo, Liwaka amesema kupitia Mfuko wa Jimbo, kiasi cha Shilingi milioni tatu kimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa jengo la kupumzikia wagonjwa katika kituo hicho, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma za afya.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano, Liwaka ameishukuru Serikali kwa kuwezesha upatikanaji wa gari hilo, huku akiipongeza Wizara ya Afya kwa mchango wake katika kufanikisha upatikanaji wa ambulance hiyo.

Kwa upande wao, wananchi wa Naipanga wameeleza kufurahishwa na ujio wa gari hilo, wakisema litasaidia kupunguza changamoto ya usafiri wa wagonjwa na kuimarisha huduma za rufaa kwa wakati.

Wamesema hatua hiyo itaongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za afya katika Kituo cha Afya Naipanga, hususan kwa wagonjwa wanaohitaji huduma katika vituo vya juu zaidi vya afya.

Posted in

Leave a comment