
Na Mwandishi Wetu, Nachingwea—Lindi
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano ya Kazi), Deus Sangu, ameweka jiwe la msingi la Jengo la Mama na Mtoto katika Zahanati ya Kijiji cha Nditi, Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea, mkoani Lindi.
Waziri Sangu ameweka jiwe hilo la msingi ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani Lindi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Sangu aliwapongeza wananchi wa Kijiji cha Nditi kwa ushiriki wao katika ujenzi wa jengo hilo, akisema hatua hiyo ni mfano mzuri wa maendeleo yanayotokana na ushirikiano kati ya wananchi na Serikali.
Aliahidi kuchangia vitanda viwili vya kujifungulia vyenye thamani ya Shilingi milioni 3.6, ili kusaidia kuboresha huduma za afya kwa mama na mtoto katika zahanati hiyo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Nachingwea, Fadhili Liwaka, alimshukuru Waziri Sangu kwa kutembelea kijiji hicho na kuweka jiwe la msingi la jengo hilo.

Liwaka alisema sekta ya afya ni miongoni mwa vipaumbele vya maendeleo katika eneo hilo, akibainisha kuwa hatua inayofuata ni ujenzi wa Kituo cha Afya ili kuendelea kuboresha huduma kwa wananchi.
Diwani wa Kata ya Nditi, Castory Joseph Mtonga, alisema awali zahanati hiyo ilikuwa na chumba kimoja pekee, hali iliyosababisha ukosefu wa faragha kwa akina mama wakati wa kujifungua na kupata huduma nyingine za uzazi.
Alisema kukamilika kwa jengo hilo jipya kutawawezesha wanawake kujifungua katika mazingira salama na yenye staha, huku akiishukuru Serikali kwa mchango wake katika kufanikisha mradi huo.
Wananchi Aisha Abdallah Hassani na Shabani Omari Juma walisema ujenzi wa Jengo la Mama na Mtoto utasaidia kumaliza changamoto ya akina mama kuchanganywa na wagonjwa wengine katika chumba kimoja, hali iliyokuwa ikikosesha faragha wakati wa kupata huduma za uzazi.
Walisema kukamilika kwa ujenzi huo kutaongeza ubora wa huduma za afya na hadhi ya huduma za uzazi katika eneo hilo.
Aidha, wananchi hao waliiomba Serikali kuendelea kuiboresha zahanati hiyo kwa kuipatia vifaa tiba muhimu, ili waweze kupata huduma zote za msingi katika kijiji chao badala ya kulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma katika Hospitali ya Mnero.

Leave a comment