Na George Gabriel, Nanyumbu

Wananchi wa Kijiji cha Mchangani, Wilaya ya Nanyumbu, wameipongeza Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu kwa kuimarisha huduma ya chakula shuleni, wakisema hatua hiyo imechangia kuboresha afya, mahudhurio na uwezo wa wanafunzi kujifunza.

Akizungumza kuhusu huduma hiyo, Ajibu Besha, mkazi wa Kijiji cha Mchangani, ameipongeza Serikali na uongozi wa shule kwa kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula wakiwa shuleni, akisema hatua hiyo imewasaidia watoto kusoma katika hali nzuri bila kukabiliwa na changamoto ya njaa.

“Tunawashukuru sana Serikali na shule kwa kuhakikisha watoto wetu wanapata chakula wakiwa shuleni. Hii inawasaidia kusoma vizuri na pia kutunza afya zao,” alisema Besha.

Kwa upande wake, Namaka Saidi, mwanafunzi wa Darasa la Nne katika shule hiyo, ameishukuru Serikali kupitia Afisa Lishe wa Wilaya kwa kuwawezesha kupata huduma ya chakula shuleni, akisema hatua hiyo inawasaidia kusoma kwa bidii wakiwa na afya njema.

“Tunawashukuru Serikali na Afisa Lishe wa Wilaya kwa kutuletea chakula shuleni. Sasa tunasoma kwa bidii kutokana na uwepo wa huduma ya chakula,” alisema Namaka.

Aidha, Kitengo cha Lishe kimeendelea kusimamia utekelezaji wa afua za lishe shuleni kwa lengo la kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula salama na chenye lishe bora, jambo linalolenga kuchangia katika kuboresha afya, ukuaji na maendeleo yao kitaaluma.

Halmashauri pia imeendelea kuhimiza uboreshaji wa mazingira ya ulaji shuleni, ikiwemo kuweka utaratibu mzuri wa wanafunzi kupata chakula katika mazingira salama, safi na yanayozingatia afya.

Posted in

Leave a comment