Na Pilastus Nyaulingo, Ushetu, Shinyanga

Halmashauri ya Ushetu kupitia Idara ya Elimu imemkabidhi Tuzo ya Heshima Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Emmanuel Cherehani, kwa kutambua mchango wake katika kuimarisha sekta ya elimu na kuunga mkono juhudi za kuboresha huduma za elimu katika halmashauri hiyo.

Tuzo hiyo ilikabidhiwa jana katika hafla iliyosisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya viongozi, watumishi wa umma na wadau wa elimu katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, kwa lengo la kuinua kiwango cha elimu kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ushetu, Hadija Kabojela, alisema tangu Cherehani aingie madarakani amekuwa akitoa ushirikiano mkubwa katika kuendeleza sekta ya elimu, ikiwemo kuisemea katika ngazi mbalimbali na kutoa motisha kwa walimu na wanafunzi.

Kabojela alisema ushirikiano huo umechangia kuimarisha juhudi za maendeleo ya elimu katika halmashauri hiyo na kuongeza hamasa kwa walimu na wanafunzi kuendelea kufanya vizuri kitaaluma.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ushetu, Gagi Lala Gagi, alisema halmashauri hiyo inajivunia ushirikiano uliopo na mbunge huyo, akieleza kuwa amekuwa mstari wa mbele kutetea maslahi ya wananchi na kuchangia upatikanaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo miradi ya sekta ya elimu.

Alisema uwekezaji katika elimu ni msingi wa maendeleo ya jamii, huku ushirikiano kati ya viongozi na wadau ukiendelea kuwa muhimu katika kuboresha huduma zinazowagusa moja kwa moja wanafunzi na walimu.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Emmanuel Cherehani, aliishukuru Idara ya Elimu pamoja na watumishi wa Halmashauri ya Ushetu kwa kutambua mchango wake katika sekta hiyo.

Alisema tuzo hiyo imempa nguvu na motisha ya kuendelea kushirikiana na halmashauri katika kuendeleza sekta ya elimu pamoja na huduma nyingine za kijamii kwa manufaa ya wananchi wa Ushetu.

Aidha, aliahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, pamoja na kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha sekta ya elimu inaendelea kupata mafanikio.

Kutolewa kwa tuzo hiyo kumeelezwa kuwa ni sehemu ya kuhamasisha ushirikiano kati ya viongozi na wadau wa maendeleo katika kuimarisha sekta ya elimu, ambayo ni msingi wa maendeleo endelevu ya jamii.

Posted in

Leave a comment