Na Cartace Ngajiro, Tanga

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imepongezwa kwa kuendelea kutekeleza sera ya bahari kwa kuimarisha ulinzi na usalama katika bandari zake nchini.
Pongezi hizo zimetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi Ali Said Bakari, alipotembelea Banda la TPA wakati wa ufunguzi wa Maadhimisho ya Siku ya Usafirishaji Majini Duniani yaliyofanyika katika Viwanja vya Kijiji cha 21, Tanga Mjini, ambapo alikuwa mgeni rasmi.
Mhandisi Bakari alisema mafanikio yanayopatikana katika sekta ya bandari yana mchango mkubwa katika kuboresha miundombinu ya bahari nchini, pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama kwa watumiaji wa bahari na shehena za wateja.
Akitoa maelezo mbele ya mgeni rasmi, Afisa Mkuu wa Masoko wa TPA, Ally Tembele, alisema mamlaka hiyo inaendelea kuthibitisha kwa vitendo utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 kwa kununua boti mbili za kisasa za doria kwa ajili ya kuimarisha ulinzi na usalama majini.

“Boti hizo ambazo ni MV Lindo na MV Lindo II, zimeongeza ulinzi na usalama kwa watumiaji wa huduma za bandari, meli pamoja na shehena za wateja,” alisema Tembele.
Alisema uwepo wa boti hizo za kisasa za doria ni sehemu ya jitihada za TPA kuhakikisha mazingira ya shughuli za kibandari yanakuwa salama na yenye ufanisi kwa wadau wote wanaotumia huduma za bandari.
TPA imeungana na taasisi nyingine zinazohusika na sekta ya bahari nchini kuadhimisha Siku ya Usafirishaji Majini Duniani, yenye kaulimbiu “Kutoka Sera hadi Utekelezaji: Kuimarisha Ubora katika Sekta ya Usafirishaji Majini.”


Leave a comment