
Na Andrea Mlwafu
Wataalamu wa elimu na mitaala kutoka Tanzania na nchi mbalimbali za Afrika wamekutana kujadili namna mifumo ya elimu barani Afrika inavyoweza kuendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia, akili bandia (AI) na mabadiliko ya mahitaji ya soko la ajira.
Hayo yamejiri katika Kongamano la Sita la Chama cha Mitaala cha Afrika (ACA 2026) lililoanza leo katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam, na linatarajiwa kuendelea hadi Septemba 25, 2026.
Kongamano hilo limewakutanisha watunga mitaala, watafiti, watunga sera, walimu, wakufunzi, wahadhiri na wanafunzi wa uzamili kutoka Tanzania, nchi nyingine za Afrika na maeneo mbalimbali duniani.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE), Dkt. Aneth Komba, amesema mabadiliko ya kiteknolojia yanaifanya Afrika kutazama upya namna mitaala inavyoandaliwa ili kuwaandaa wanafunzi wenye ujuzi unaohitajika katika karne ya 21.

Amesema elimu haipaswi kuishia katika kumpa mwanafunzi maarifa ya darasani pekee, bali inapaswa kumjengea uwezo wa kutumia maarifa hayo kutatua changamoto zinazokabili jamii.
“Kongamano hili pia linatoa nafasi kwa Tanzania kushirikisha uzoefu wake katika mageuzi ya elimu, ikiwemo utekelezaji wa sera na maboresho ya mitaala yanayoendelea nchini,” amesema Dkt. Komba.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha Mitaala cha Afrika (ACA), Dkt. Gertrude Namubiru, amesema mageuzi ya mitaala barani Afrika hayapaswi kuangalia teknolojia pekee, bali yanapaswa kuzingatia pia historia, utamaduni na mazingira halisi ya jamii za Afrika.

Amesema elimu inapaswa kuwasaidia watoto wa Afrika kuielewa jamii inayowazunguka na kupata uwezo wa kushiriki katika kuibadilisha, badala ya kutegemea mifumo iliyotengenezwa kwa kuzingatia mazingira ya nje ya bara hilo.
Miongoni mwa maeneo yatakayojadiliwa katika kongamano hilo ni matumizi ya AI na teknolojia nyingine katika ufundishaji na ujifunzaji, maandalizi ya walimu, elimu jumuishi, mifumo ya upimaji, pamoja na namna ya kufanya mitaala iendane na mahitaji ya mwanafunzi wa karne ya 21.
Aidha, kongamano hilo linatarajiwa kutoa Azimio la Dar es Salaam kuhusu Mabadiliko ya Elimu Afrika, pamoja na kupitisha rasimu ya mfumo wa Afrika wa maendeleo na maboresho ya mitaala.
Mfumo huo unatarajiwa kuendana na Ajenda ya Umoja wa Afrika 2063 pamoja na Lengo la Nne la Maendeleo Endelevu (SDG 4), linalolenga kuhakikisha upatikanaji wa elimu bora, jumuishi na yenye usawa.
Kongamano hilo linaendelea jijini Dar es Salaam hadi Septemba 25, likiwa na lengo la kuimarisha ushirikiano miongoni mwa wataalamu wa elimu na kuweka mapendekezo yatakayosaidia mifumo ya elimu ya Afrika kukabiliana na mabadiliko ya kiteknolojia na kijamii.

Leave a comment