Na Pilastus Nyaulingo, Dodoma

Wadau wa sekta ya kilimo na mazingira wameeleza kuwa kilimo mseto cha miti na mazao kinaweza kuwa fursa muhimu kwa vijana kujiajiri, kuongeza kipato na kuchangia kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Kauli hiyo imetolewa katika mkutano wa wadau uliofanyika Dodoma, pembezoni mwa maonesho ya Nane Nane, ambapo washiriki walijadili namna ya kuendeleza kilimo mseto kama njia ya kuboresha maisha ya jamii na kuongeza fursa za kiuchumi kwa vijana.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Nchi wa Vi Agroforestry Tanzania, Martha Olotu, alisema kilimo mseto kina fursa mbalimbali za kiuchumi kwa vijana, huku kikiendelea kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto zinazoikabili sekta ya kilimo na mazingira.

Alisema vijana wanapaswa kupewa nafasi kubwa zaidi katika sekta hiyo kwa kuwa wanaweza kutumia maarifa, teknolojia na ubunifu kuanzisha shughuli zinazohusiana na kilimo mseto na kujenga vyanzo vya kipato.

“Uwekezaji katika kilimo mseto utasaidia vijana kujenga ajira na biashara zinazohusiana na uzalishaji wa mazao, miti na shughuli nyingine za kilimo zinazolenga kuhifadhi mazingira,” alisema Olotu.

Kwa upande wake, mmoja wa maafisa walioshiriki katika mjadala huo, Edna Paul, alisema kilimo mseto kina nafasi muhimu katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuboresha uzalishaji wa chakula.

Alisema mfumo huo huwezesha kuboresha rutuba ya udongo, kuongeza uzalishaji wa chakula na kuchangia kupunguza changamoto za utapiamlo katika jamii.

Alisema kuunganisha miti na mazao katika mifumo ya kilimo kutasaidia wakulima kutumia ardhi kwa ufanisi zaidi huku wakilinda mazingira na kujenga uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Mkurugenzi wa Civil Social Protective Foundation na mshirika wa Vi Agroforestry, Nemesi Kiliya, alisema kuna umuhimu wa ushirikiano wa wadau mbalimbali katika kukuza kilimo mseto nchini.

Alisema mpango wa kuanzisha jukwaa la kitaifa la wadau wa kilimo mseto utasaidia kuimarisha ushirikiano, kubadilishana uzoefu na kuongeza uwekezaji katika sekta hiyo kwa njia endelevu.

Alisema jukwaa hilo pia litasaidia kuwaunganisha vijana, wakulima, mashirika na taasisi zinazohusika na sekta za kilimo na mazingira.

Mkazi wa Nzuguni, Dodoma, Aidani Naftari, alisema kilimo mseto ni fursa inayoweza kuwasaidia vijana kujipatia kipato huku wakishiriki katika uhifadhi wa mazingira.

“Kwa mtazamo wangu, vijana wengi tunatafuta ajira, lakini si lazima kila mtu aajiriwe kwenye ofisi. Tukipata elimu, mtaji na teknolojia sahihi, tunaweza kutumia kilimo na upandaji miti kujiajiri na kujenga maisha yetu,” alisema Naftari.

Alisema serikali na wadau wanapaswa kuendelea kuwawezesha vijana ili fursa hiyo isiishie kwenye mijadala pekee, bali iwe chanzo cha ajira na maendeleo kwa jamii.

Posted in

Leave a comment