
Na George Gabriel
Wananchi wa Kijiji cha Masuguru, Kata ya Masuguru, Wilaya ya Nanyumbu, wamempongeza Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, kwa kutimiza ahadi yake ya kuchangia madawati 13 kwa ajili ya Shule ya Msingi Masuguru.
Pongezi hizo zilitolewa hivi karibuni na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu na Diwani wa Kata ya Masuguru, Benjamin Raphael Masimbo, pamoja na viongozi mbalimbali wa Kata na Kijiji hicho, wakati wa zoezi la kukabidhi madawati hayo kwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Masuguru, Fariji Rweyemamu.
Msaada huo umetokana na ahadi iliyotolewa na Waziri Kapinga Agosti 10, 2026, wakati alipokwenda kukagua Mradi wa Maji wa Mto Ruvuma hadi Mangaka, ambapo alichangia shilingi milioni moja (TSh 1,000,000) kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wa madawati hayo.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa kwa madawati hayo, Ashura Mfaume, mkazi wa Kijiji cha Masuguru, alimpongeza Waziri Kapinga kwa kutimiza ahadi yake na kumshukuru kwa kuendelea kuwa karibu na wananchi.

“Tunamshukuru sana Mhe. Waziri kwa kutimiza ahadi yake. Madawati haya yatasaidia sana wanafunzi wetu na kupunguza changamoto ya kukaa chini wakati wa masomo,” alisema Bi. Ashura.
Kwa upande wake, Mustapha Chikomela, mwananchi wa Kijiji cha Masuguru, alimpongeza Waziri Kapinga kwa kutekeleza ahadi hiyo kwa vitendo, akisema hatua hiyo ni mfano wa ushirikiano kati ya viongozi na wananchi katika kuboresha mazingira ya elimu.
Aidha, uongozi wa Kijiji cha Masuguru, kwa kushirikiana na viongozi wa Kata ya Masuguru, ulitoa shukrani kwa Serikali na viongozi kwa kuendelea kutoa ushirikiano na misaada mbalimbali yenye lengo la kuleta maendeleo kwa wananchi.

Leave a comment