Na George Gabriel

Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, Christopher Magala, amefungua mafunzo ya siku moja kwa madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu, yenye lengo la kuwajengea uwezo katika kutekeleza majukumu yao, hususan usimamizi wa fedha na rasilimali za umma.

Akizungumza katika mafunzo hayo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri, Magala alisema madiwani wana wajibu wa kusimamia kikamilifu maslahi ya wananchi waliowachagua kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya viongozi wa umma, pamoja na kuepuka vitendo vinavyoweza kusababisha mgongano wa maslahi.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Mkoa wa Mtwara, Shedrack Mrema, alisema ni muhimu vikao na mabaraza ya madiwani kujadili kwa kina hoja zinazoibuliwa na CAG ili kuhakikisha Serikali inawajibika kutoa majibu na kuchukua hatua stahiki.

Alisema hatua hiyo itasaidia kuimarisha uwajibikaji na kuongeza kasi ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa wananchi.

Miongoni mwa mada zilizowasilishwa katika mafunzo hayo ni wajibu wa Baraza la Madiwani katika kusimamia rasilimali za Halmashauri, pamoja na wajibu na majukumu ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Mada nyingine zilihusu mwenendo wa utekelezaji wa mapendekezo ya ukaguzi, pamoja na uchambuzi wa taarifa za fedha na miradi ya maendeleo.

Kwa upande wao, madiwani Benjamini Masimbo na Salvatory Lyimo walipongeza kutolewa kwa mafunzo hayo, wakisema yamewasaidia kuongeza uelewa na uwezo katika kutekeleza majukumu yao ya udiwani.

Madiwani hao waliahidi kutumia maarifa waliyoyapata kupitia mafunzo hayo kuimarisha usimamizi wa Halmashauri na rasilimali zake, ili kuhakikisha zinatumika kwa ufanisi na kuleta tija na manufaa kwa wananchi.

Posted in

Leave a comment