
Na Abel Mwakingwe
Wananchi wa Makunganya, Morogoro, sasa wana unafuu wa upatikanaji wa maji safi na salama baada ya kisima chenye thamani ya Shilingi milioni 38 kukabidhiwa kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa ajili ya matumizi ya jamii na shughuli za uhifadhi.
Kisima hicho, kilichotolewa na Mkwawa Group of Campaign na kukabidhiwa Oktoba 1, 2026, kinatarajiwa kupunguza changamoto iliyowakabili wakazi wa eneo hilo ambao awali walilazimika kutembea umbali wa hadi kilomita 10 kutafuta maji.
Mbali na kusaidia jamii, kisima hicho kinatarajiwa kuimarisha shughuli za uhifadhi katika eneo la Makunganya, ikiwemo uzalishaji, uoteshaji na uangalizi wa miche ya miti.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, mkazi wa Makunganya, Recho Mapenza, amesema upatikanaji wa kisima hicho umepunguza changamoto ya wananchi kutembea umbali mrefu kutafuta maji.
Amesema wananchi wako tayari kushirikiana na TFS kuhakikisha kisima hicho kinatunzwa na mazingira yanayowazunguka yanalindwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uzalishaji wa Kiwanda cha Mkwawa, David Mayunga, amesema kampuni hiyo imeamua kushirikiana na TFS kutokana na umuhimu wa shughuli za uhifadhi zinazotekelezwa katika eneo hilo.

Mayunga amewataka wananchi wanaotumia kisima hicho kuhakikisha wanakitunza na kukilinda ili kiendelee kutoa huduma kwa muda mrefu.
Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Morogoro na Mkuu wa Kituo cha Uzalishaji Mbegu za Miti, Mohamed Msalu, amesema kisima hicho kimewasili wakati ambao TFS inaendelea na mkakati wa kuongeza uzalishaji wa mbegu na miche ya miti.
Amesema upatikanaji wa maji utasaidia kupunguza changamoto iliyokuwa ikikabili jamii inayozunguka shamba hilo, huku ukiwezesha shughuli zinazohusiana na uzalishaji wa miche na uhifadhi kufanyika kwa ufanisi zaidi.
Kwa mujibu wa Msalu, miundombinu hiyo pia inaweza kuimarisha ushirikiano kati ya jamii inayozunguka eneo hilo na wahifadhi katika kulinda mazingira na kutekeleza shughuli za uhifadhi.
Ametoa shukrani kwa Mkwawa Group of Campaign kwa kushirikiana na Serikali katika kuunga mkono juhudi za uhifadhi wa misitu na utalii ikolojia.
Kisima hicho sasa kinatarajiwa kuwa sehemu ya miundombinu muhimu katika eneo la Makunganya, kikikidhi mahitaji ya maji ya jamii inayozunguka eneo hilo na wakati huo huo kusaidia shughuli za uhifadhi, hususan uzalishaji na uoteshaji wa miche ya miti.
Kwa wananchi waliokuwa wakitembea hadi kilomita 10 kutafuta maji, huduma hiyo inamaanisha kupunguzwa kwa muda na umbali waliokuwa wakitumia kutafuta maji, huku TFS ikipata nyenzo ya kusaidia shughuli zake za uhifadhi.


Leave a comment