
Na Cartace Ngajiro – Tanga
Bandari nchini zimeendelea kuwa chanzo muhimu cha mapato ya Serikali, huku kodi za forodha zinazokusanywa kupitia bandari zikichangia wastani wa takribani asilimia 40 ya mapato yote ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021 hadi 2024/2025.
Kutokana na umuhimu huo, Serikali imesema itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya bandari, vifaa na usalama wa vyombo vya majini ili kuongeza ufanisi, kupunguza gharama na muda wa usafirishaji.
Akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Usafiri Majini Duniani yaliyofanyika hivi karibuni katika Viwanja vya Kijiji cha 21, mkoani Tanga, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Mwakiposa Kihenzile (Mb.), alisema Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya bandari, huduma za mizigo na abiria pamoja na usalama wa vyombo vya majini.
Akitoa maelezo mbele ya mgeni rasmi, Mwakilishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Meneja wa Bandari ya Tanga, Salehe Mbega Salehe, alisema kiwango cha shehena kilichohudumiwa na TPA kimeongezeka kutoka tani 32,753,618 katika mwaka wa fedha 2024/2025 hadi tani 39,898,913 mwaka 2025/2026.

Alisema ongezeko hilo ni sawa na asilimia 21.8, huku TPA ikitarajia kuhudumia tani 43,372,285 katika mwaka wa fedha 2026/2027.
Mbega alisema TPA imechukua hatua za kuongeza wataalamu katika fani ya usafiri wa majini (Marine), ambapo wafanyakazi 25 wamepelekwa nje ya nchi kwa ajili ya mafunzo katika fani mbalimbali zinazohusiana na sekta hiyo.
Alisema wataalamu hao wanatarajiwa kumaliza masomo yao mwaka 2027.
Kwa upande wa vifaa, alisema TPA imeongeza vifaa na vyombo vya baharini, ikiwemo Tug Boat saba zenye teknolojia ya kisasa pamoja na boti mbili za doria—moja kwa ajili ya ukanda wa Bahari ya Hindi na nyingine katika Ziwa Victoria.
Hatua hizo zinalenga kuongeza uwezo wa bandari kuhudumia meli, kuimarisha usalama na kuboresha ufanisi wa shughuli za usafirishaji wa majini.
Kihenzile alisema Serikali itaendelea kuwekeza katika bandari ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya usafirishaji wa mizigo na abiria.
Alisema uwekezaji huo unalenga kuhakikisha huduma za bandari zinaendelea kuwa na ufanisi, huku usalama wa meli na vyombo vingine vya majini ukiimarishwa.
Ongezeko la shehena iliyohudumiwa na TPA kutoka tani milioni 32.7 hadi milioni 39.9 ndani ya mwaka mmoja linaonyesha kuongezeka kwa shughuli za bandari, jambo linalohitaji miundombinu na wataalamu wenye uwezo wa kukidhi mahitaji hayo.

Leave a comment