Na George Gabriel – Nanyumbu

Wananchi wa Wilaya ya Nanyumbu wameanza kuchukua hatua za mapema kukabiliana na uwezekano wa mvua za El Nino, ikiwemo kuhakikisha mifereji ya maji inakuwa wazi na kuondoa vitu vinavyoweza kuziba njia za maji ili kupunguza hatari ya mafuriko.

Wananchi hao wamesema wameelewa umuhimu wa kutosubiri madhara yatokee, bali kujiandaa mapema kwa kulinda familia, mali, mifugo, mashamba na maeneo yao dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na mvua kubwa.

Akizungumza wakati wa ziara katika vijiji vya Chimika na Mpwaha vinavyohusika na Hifadhi ya Lukwika-Lumesule, Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, Christopher E. Magala, aliwahimiza wananchi kuendelea kuchukua tahadhari na kufuatilia taarifa za hali ya hewa pamoja na maelekezo yanayotolewa na mamlaka husika.

Magala alisema mvua za El Nino zinaweza kuambatana na mvua nyingi zinazoweza kusababisha mafuriko, uharibifu wa makazi, mashamba, mifugo, miundombinu na shughuli za kiuchumi.

Aliwataka wananchi kuimarisha maandalizi kwa kuhakikisha mifereji ya maji inakuwa wazi, kuondoa taka na vitu vingine vinavyoweza kuzuia mtiririko wa maji, pamoja na kuwa makini katika maeneo yanayoweza kuathiriwa na mafuriko.

Juma Mponda na Shaibu Ayubu, wakazi wa eneo hilo, walisema elimu na maelekezo yaliyotolewa na Serikali yamewasaidia kuelewa umuhimu wa kuchukua tahadhari mapema.

Mponda alisema wananchi wataendelea kufuatilia taarifa za hali ya hewa na kuchukua hatua pindi wanapoona dalili za hatari, huku wakishirikiana na Serikali katika kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.

“Ni muhimu kujiandaa mapema badala ya kusubiri madhara yatokee. Tutaendelea kuhakikisha familia, mifugo na mali zetu ziko katika hali salama,” alisema Mponda.

Naye Ayubu alisema wananchi wamepokea wito huo kwa uzito na wataendelea kuhamasishana katika maeneo yao ili kuhakikisha kila mmoja anafanya maandalizi ya mapema.

Alisisitiza umuhimu wa kuzingatia taarifa zinazotolewa na mamlaka husika kuhusu hali ya hewa pamoja na kufuata maelekezo ya wataalamu wakati wote wa msimu wa mvua.

Katika ziara hiyo, wananchi pia walipatiwa elimu kuhusu ujirani mwema na umuhimu wa uhifadhi wa wanyamapori, pamoja na namna ya kujikinga dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori.

Aidha, walihimizwa kutoa taarifa mapema wanapokutana na changamoto zinazohusiana na wanyamapori ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.

Wananchi hao pia wamewataka wakazi wengine wa maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Nanyumbu kuimarisha usafi wa mazingira na kuondoa vitu vinavyoweza kuzuia mtiririko wa maji, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na mvua kubwa.

Posted in

Leave a comment