
Na Pilastus Nyaulingo
Kampuni ya Yas Tanzania imezindua huduma ya Yas Fiber jijini Dodoma, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa intaneti ya kasi kwa kaya, wafanyabiashara na taasisi katika mji unaoendelea kukua kwa kasi.
Huduma hiyo ya nyuzi-optiki kwa sasa inapatikana katika maeneo ya Ilazo, Ipagala, Swaswa, Mjini Kati na Barabara za Namba, huku kampuni hiyo ikieleza kuwa itaendelea kupanua huduma katika maeneo mengine kulingana na mahitaji ya wananchi.
Uzinduzi huo ulifanyika jijini Dodoma hivi karibuni na kuhudhuriwa na viongozi wa Serikali, wateja pamoja na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya jiji, ukiwa sehemu ya juhudi za kuongeza miundombinu ya mawasiliano ya kisasa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Yas Fiber, Maxime Woimant, alisema kampuni hiyo inalenga kuchochea mabadiliko ya kidijitali Dodoma kwa kuhakikisha wakazi na wafanyabiashara wanapata muunganisho wa uhakika utakaowawezesha kufanya kazi, kujifunza na kupata huduma za kidijitali kwa ufanisi zaidi.

“Tunajitolea kusaidia mabadiliko ya kidijitali ya Dodoma kwa kutoa muunganisho wa kuaminika ambao utawawezesha wakazi na wafanyabiashara kufanya kazi, kujifunza, kuendesha shughuli kwa ufanisi zaidi na kupata huduma za kidijitali,” alisema Woimant.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Jabir Shekimweri, aliyeshiriki katika uzinduzi huo, alisisitiza umuhimu wa kuwa na miundombinu ya kidijitali yenye uhakika wakati Dodoma ikiendelea kupanuka.
Shekimweri alisema upanuzi wa huduma za mawasiliano unaweza kufungua fursa zaidi za kiuchumi na kijamii kupitia uchumi wa kidijitali.
Katika uzinduzi mwingine wa huduma za Yas jijini Dodoma mwezi Machi 2026, Shekimweri alisema upanuzi wa huduma za mawasiliano unaweza kusaidia kuongeza shughuli za kiuchumi, kurahisisha upatikanaji wa huduma na kuimarisha muunganisho kwa wakazi.
Kwa upande wake, Yas Tanzania imesema uzinduzi wa Yas Fiber unalenga pia kuongeza fursa za kujifunza mtandaoni, kuwasaidia wajasiriamali kufikia masoko mapya, kurahisisha uendeshaji wa biashara na kuongeza upatikanaji wa huduma za kidijitali kwa kaya.
Hatua hiyo inakuja wakati matumizi ya intaneti nchini yakiendelea kuongezeka. Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), hadi Juni 2025 kulikuwa na watumiaji wa intaneti 54,078,530 nchini, huku teknolojia za 3G, 4G na 5G zikiendelea kuenea katika maeneo mbalimbali.
Leave a comment