Na Abel Mwakingwe

Wananchi wa Wilaya ya Nkansi na Manispaa ya Sumbawanga wanatarajiwa kupata huduma bora zaidi za afya baada ya Zahanati za Chala na King’ombe kupatiwa vifaa tiba vyenye thamani ya jumla ya Sh milioni 312.

Zahanati ya Chala imepokea vifaa vyenye thamani ya Sh milioni 267, huku Zahanati ya King’ombe katika Manispaa ya Sumbawanga ikipokea vifaa vya Sh milioni 45.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Rukwa, Jacqueline Mzindakaya, alisema vifaa hivyo vitaongeza uwezo wa zahanati hizo kutoa huduma za uchunguzi na matibabu, hususan kwa wanawake wajawazito na watoto.

“Miongoni mwa faida kubwa ya vifaa hivi ni kusaidia kuimarisha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi pamoja na kupunguza vifo vya wanawake wajawazito na watoto,” alisema Mzindakaya.

Vifaa hivyo vilivyotolewa kupitia mgao wa Mradi wa TCHMP vinajumuisha mashine za kidijitali za kupima shinikizo la damu, vifaa vya kufuatilia mapigo ya moyo wa mtoto tumboni, mashine za kufuatilia hali ya wagonjwa, vifaa vya kusaidia kujifungua, viti vya magurudumu, friji za kuhifadhia dawa na vitanda vya kujifungulia.

Mzindakaya aliishukuru Serikali kwa kupeleka vifaa hivyo, akisema vitasaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa vifaa tiba na kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma katika zahanati hizo.

Vifaa hivyo vinatarajiwa kuongeza ufanisi wa huduma za afya, hasa kwa wanawake wajawazito na watoto wanaofika katika vituo hivyo.

Posted in

Leave a comment