Na Iddy Mziray, Songea

Wazee mkoani Ruvuma wameiomba Serikali kuhakikisha haki zao zinatekelezwa, ikiwamo kupata matibabu bure na kipaumbele hospitalini, kulipwa pensheni kwa wakati na kulindwa dhidi ya unyanyasaji.

Wazee hao walitoa kilio hicho wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yaliyofanyika Kata ya Lizaboni, Songea, ambapo walifanya maandamano mafupi kutoka Shule ya Msingi Kiblangoma hadi eneo la maadhimisho.

Miongoni mwa kero walizowasilisha kwa Meya wa Manispaa ya Songea, Abraham Mbunda, ni kuchelewa kwa pensheni, foleni ndefu hospitalini na ukosefu wa fursa za mikopo na misaada ya kuwawezesha kujitegemea.

“Kuna wazee tumefanya kazi miaka 30 lakini pensheni yetu inachelewa miezi mitatu hadi sita. Tunakula nini?” alihoji mmoja wa wazee.

Waliomba pia kuwepo kwa dirisha maalum la huduma za afya kwa wazee ili waweze kupata matibabu kwa urahisi na bila kusubiri muda mrefu.

Akijibu maombi hayo, Meya Mbunda alisema Manispaa itahakikisha wazee wanapewa kipaumbele katika vituo vya afya na kuahidi kufuatilia suala la malipo ya pensheni.

“Tutahakikisha wazee wote wanapata kipaumbele kwenye vituo vyetu vya afya,” alisema Mbunda.

Mbunda aliahidi pia kufikisha kero hizo katika Baraza la Madiwani na kwa Mkuu wa Mkoa kwa ajili ya hatua zaidi.

Posted in

Leave a comment