
Na Grace Mwakalinga
Jumla ya wanafunzi 1,591,064 wanatarajiwa kuanza kufanya Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne kesho, Oktoba 5, hadi Oktoba 6, 2026.
Kati yao, wavulana ni 764,284, sawa na asilimia 48, huku wasichana wakiwa 826,780, sawa na asilimia 51.9.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Profesa Said Mohamed, amesema upimaji huo ni muhimu katika kubaini kiwango cha wanafunzi katika kumudu stadi mbalimbali za msingi.
Amesema upimaji huo unalenga kubaini kiwango cha wanafunzi katika kusoma, kuandika, kutumia lugha ya Kiingereza, kuhesabu pamoja na umahiri katika masomo ya lazima, ikiwamo Kiswahili.
Wakati huo huo, jumla ya wanafunzi 1,827,367 wamesajiliwa kufanya Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Pili, utakaofanyika Oktoba 7 na 8, 2026.
Kati yao, wavulana ni 906,545, sawa na asilimia 49.6, huku wasichana wakiwa 920,822, sawa na asilimia 50.4.
Kwa upande wa Kidato cha Pili, wanafunzi 794,713 wameorodheshwa kufanya upimaji mwaka huu. Kati yao, wanafunzi 786,163 ni wa shule, huku watahiniwa 8,550 wakiwa wa kujitegemea.
Kati ya wanafunzi hao, 781,127 watafanya upimaji katika Mkondo wa Jumla, huku 5,036 wakifanya katika Mkondo wa Amali, ambao ulianza kutahiniwa mwaka 2025 kwa kuzingatia Sera ya Elimu na Mafunzo.
Aidha, wanafunzi 1,162 wenye mahitaji maalum wamesajiliwa kufanya upimaji huo. Kati yao, 939 wana uoni hafifu, 78 hawaoni, 56 wana uziwi, 13 wana ulemavu wa akili na 76 wana ulemavu wa viungo.
Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili utafanyika kuanzia Oktoba 12 hadi 23, 2026.
Leave a comment