Na Grace Mwakalinga

Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linawashikilia watu wawili kufuatia tukio la kuwashambulia wananchi sita katika Kitongoji cha Kiloweko, Kijiji cha Kwazoka, Kata ya Vigwaza.

Watuhumiwa hao, ambao ni wafugaji wa jamii ya Kimasai na majina yao yamehifadhiwa, wanadaiwa kuwa sehemu ya kundi lililowavamia baadhi ya wajumbe wa Chama cha Ushirika cha Umwagiliaji Ruvu (CHAURU) pamoja na Afisa Tarafa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, amesema tukio hilo lilitokea wakati Afisa Tarafa na wajumbe wa CHAURU walipokuwa wakipita katika eneo hilo kuwapatia wafugaji notisi ya kuondoka katika eneo la shamba la chama hicho walilodaiwa kulivamia.

Kwa mujibu wa Kamanda Morcase, chanzo cha tukio hilo kinadaiwa kuwa ni baadhi ya wafugaji kupinga kupewa notisi ya kuondoka katika eneo hilo, wakidai kuwa wamekuwa wakiishi hapo kwa muda mrefu.

Amesema baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi lilifanya operesheni kwa kushirikiana na viongozi wa wafugaji pamoja na baadhi ya wananchi, ambapo lilifanikiwa kupata mwili wa bunduki na pikipiki yenye namba za usajili MC 136 CYK, vilivyochukuliwa siku ya tukio.

Vurugu katika shamba la CHAURU zimekuwa zikitokea mara kwa mara kutokana na mvutano kati ya wakulima na wafugaji. Wakulima wamekuwa wakiwatuhumu wafugaji kulisha mifugo yao katika eneo la shamba hilo la umwagiliaji na kusababisha uharibifu wa miundombinu.

Posted in

Leave a comment