
Na Abel Mwakingwe
Watoto wenye mahitaji maalum wilayani Simanjiro, Manyara, wamepatiwa vitimwendo saba vitakavyowasaidia kuwa na uhuru zaidi katika kufanya shughuli zao za kila siku, huku pia vikitumika kupunguza changamoto kwa wazazi na walezi wanaowabeba wanapowapeleka shule na katika shughuli nyingine.
Msaada huo umetolewa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Qwaray, ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Manyara, katika hatua inayolenga kuwawezesha watoto hao kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kupata elimu kwa urahisi zaidi.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vitimwendo hivyo jana, Qwaray amesema watoto wenye mahitaji maalum wanahitaji ushirikiano wa jamii ili waweze kupata elimu, kuendeleza vipaji na uwezo wao, pamoja na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii.
Alisema amekuwa akiwakumbuka watoto hao kila anapopata nafasi ya kuwasaidia, akisisitiza kuwa kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum ni sehemu ya kujenga mazingira bora ya kuishi na kushiriki katika jamii.

Kwa mujibu wa Qwaray, vitimwendo hivyo vitasaidia kupunguza changamoto wanazokutana nazo wazazi na walezi ambao wakati mwingine hulazimika kuwabeba watoto wenye ulemavu wanapowapeleka shuleni au katika shughuli mbalimbali.
“Vitimwendo hivi vitasaidia kupunguza mzigo kwa wazazi na walezi ambao wamekuwa wakiwabeba watoto wao wanapokwenda shule na maeneo mengine,” alisema Qwaray.
Aidha, aliwataka watoto waliopokea msaada huo kuvitunza na kuvitumia kwa uangalifu ili viweze kuwasaidia kwa muda mrefu.
Qwaray pia ametoa wito kwa jamii kuacha kuwaficha watoto wenye mahitaji maalum, badala yake kuwapa fursa ya kupata elimu, kushiriki katika shughuli za kijamii na kuendeleza uwezo wao.
Kwa upande wao, madiwani wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) katika Halmashauri ya Simanjiro wamempongeza Qwaray kwa hatua hiyo, huku wakitoa wito kwa viongozi na wadau wengine kuunga mkono juhudi za kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalum.
Baadhi ya wazazi waliopokea msaada huo wamemshukuru Qwaray, wakisema vitimwendo hivyo vitawasaidia watoto wao kuwa na uhuru zaidi wa kushiriki katika shughuli mbalimbali na kupunguza changamoto ya kuwabeba, hasa wanapokwenda shule.

Leave a comment