Na Mwandishi Wetu, Nachingwea – Lindi

Chama Kikuu cha Ushirika cha Runali Ltd, kinachohudumia wakulima katika Wilaya za Ruangwa, Nachingwea na Liwale, kimeweka mikakati ya kuboresha usimamizi na uendeshaji wa ununuzi na uuzaji wa zao la korosho katika msimu wa 2026/2027.

Mikakati hiyo imejadiliwa katika kikao kazi cha maandalizi ya msimu wa korosho 2026/2027 kilichofanyika katika ukumbi uliopo kwenye jengo la Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, mkoani Lindi.

Kikao hicho kimewakutanisha wadau mbalimbali wanaohusika katika mnyororo wa thamani wa zao la korosho, wakiwemo wawakilishi wa taasisi za fedha, Bodi ya Korosho Tanzania, sekta ya usafirishaji, waendesha maghala, maafisa kilimo, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), mitandao ya simu pamoja na Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mohamed Hassan Moyo, aliyekuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Adam Kigoma Ali Malima, amewataka wadau wote wanaohusika katika mnyororo wa thamani wa korosho kuwa waadilifu na kuhakikisha wakulima wanahudumiwa ipasavyo.

Moyo amesema ushirikiano na uadilifu wa wadau ni muhimu katika kuhakikisha wakulima wanapata manufaa stahiki kutokana na mazao yao, jambo ambalo litasaidia kuongeza kipato na thamani ya zao la korosho.

“Wadau wote mnaohusika katika mnyororo huu wa thamani mnatakiwa kuwa waadilifu ili kuhakikisha wakulima wanahudumiwa ipasavyo na kupata thamani halisi ya mazao yao,” alisema Moyo.

Kwa upande wake, Mrajisi Msaidizi wa Mkoa wa Lindi, Kenneth Shemdoe, amewataka wadau wote kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na uwajibikaji ili kuhakikisha mchakato wa mauzo ya mazao ya wakulima unasimamiwa kikamilifu.

Shemdoe amesema uwajibikaji wa kila mdau katika hatua mbalimbali za mnyororo wa thamani ni msingi wa kuhakikisha msimu wa korosho unaendeshwa kwa ufanisi na kwa manufaa ya mkulima.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Gudluck Mlinga, ametoa onyo kali kwa watu watakaohusika na ununuzi au uuzaji wa korosho zisizokidhi viwango, akisema hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Aidha, amewataka wakulima kuendelea kufuata taratibu bora za kuhifadhi fedha wanazopata kutokana na mauzo ya mazao yao, hususan kutumia huduma za benki, ili kuepuka matumizi holela na yasiyo na tija.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Runali Ltd, Odas Mpunga, amewataka wadau wote kuwa waadilifu katika msimu wa mauzo ya korosho wa 2026/2027, akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha wakulima wanapata malipo yao kwa wakati.

Mpunga amesema Runali Ltd itaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha upatikanaji wa vifungashio, uhifadhi na ulinzi wa ubora wa korosho, pamoja na kuimarisha mifumo ya usimamizi wa mauzo ya mazao ya wakulima.

Amesema hatua hizo ni muhimu katika kuhakikisha mnyororo mzima wa thamani wa zao la korosho unaendeshwa kwa ufanisi na bila changamoto, huku mkulima akiwa mnufaika mkuu wa shughuli za biashara ya zao hilo.

Kikao hicho ni sehemu ya maandalizi ya Runali Ltd kuhakikisha msimu wa korosho 2026/2027 unaendeshwa kwa uwazi, uwajibikaji na uadilifu, kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa, kwa lengo la kuongeza tija na kipato kwa wakulima wa korosho katika Wilaya za Ruangwa, Nachingwea na Liwale.

Posted in

Leave a comment