Na Iddy Mziray, Songea – Ruvuma

Mwekezaji na aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Madaba, Joseph Mhagama, ambaye ni mmiliki wa kampuni ya SOAGRO, ameomba Serikali imuongezee eneo la uwekezaji katika Kata ya Muhukuru Lilai, Wilaya ya Songea Vijijini, mkoani Ruvuma.

Mhagama alitoa ombi hilo hivi karibuni kwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Kaspar Kaspar Mmuya, aliyefanya ziara ya kikazi katika eneo hilo la uwekezaji.

Mhagama, ambaye kwa sasa anamiliki shamba la mitamba lenye ukubwa wa hekta 1,000 katika eneo la Muhukuru Lilai, ameomba kuongezewa hekta 3,679.7 ili kufikisha jumla ya hekta 4,679.7 kwa ajili ya kupanua uwekezaji wake.

Akizungumza mbele ya Naibu Waziri Mmuya, Mhagama alisema eneo hilo la ziada analoomba litatumika kuendeleza ufugaji wa kisasa wa ng’ombe, mbuzi na kondoo, pamoja na kuanzisha kiwanda cha kuchakata nyama.

“Mheshimiwa Naibu Waziri, ninaomba Serikali iniongezee hekta 3,679.7 kutoka hekta 1,000 nilizonazo sasa. Dhamira yangu ni kuongeza uwekezaji katika sekta ya mifugo na hatimaye kuanzisha kiwanda cha kuchakata nyama hapa hapa Muhukuru Lilai,” alisema Mhagama.

Alisema kiwanda hicho kitakuwa na manufaa kwa wananchi wa Songea Vijijini kwa kuongeza thamani ya mifugo inayozalishwa na wafugaji wa maeneo hayo, huku pia kikiwapatia soko la uhakika.

Mhagama alisema iwapo Serikali itampatia eneo hilo la ziada, atawekeza kikamilifu na kuhakikisha wananchi wa Kata ya Muhukuru Lilai wananufaika moja kwa moja kupitia fursa mbalimbali zitakazotokana na uwekezaji huo.

Alizitaja fursa hizo kuwa ni pamoja na ajira za moja kwa moja shambani na kiwandani, ajira za msimu, mafunzo ya ufugaji bora na wa kisasa, pamoja na kuboresha miundombinu ya kijamii katika kata hiyo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Kaspar Kaspar Mmuya, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika ziara hiyo, alitembelea na kujionea shamba hilo la uwekezaji na kusikiliza maombi ya mwekezaji.

Wananchi wa Muhukuru Lilai waliojitokeza kwa wingi kumlaki Naibu Waziri walimuomba kuishauri Serikali kuridhia ombi la mwekezaji huyo, wakisema uwekezaji huo utachochea maendeleo na kuchangia ukombozi wa kiuchumi, hususan kwa vijana wanaokosa ajira katika eneo hilo.

Posted in

Leave a comment