
Na Abel Mwakingwe
Tanzania inalenga kukusanya Sh trilioni 36.99 kutokana na kodi katika mwaka wa fedha 2026/27, huku Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, akisisitiza matumizi ya teknolojia kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato na kurahisisha ulipaji kodi.
Ndejembi alisema matumizi ya teknolojia katika usimamizi wa kodi ni muhimu katika kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani na kupunguza vikwazo kwa walipa kodi wanaofuata sheria.
Alisema hayo jana alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika ufunguzi wa Mkutano wa 46 wa Chama cha Wasimamizi wa Kodi wa Jumuiya ya Madola (CATA), unaofanyika katika Ukumbi wa Gran Melia jijini Arusha.
Alisema katika bajeti ya mwaka 2026/27, mapato ya ndani yanatarajiwa kugharamia takribani asilimia 74.2 ya Bajeti ya Taifa, akisisitiza kuwa matumizi ya rasilimali za ndani, hususan mapato ya kodi, ni muhimu katika kugharamia huduma za umma, miundombinu, uwekezaji wenye tija na kuimarisha kujitegemea kiuchumi.
“Ongezeko endelevu la mapato linahitaji uchumi kukua, idadi ya walipa kodi kuongezeka, wananchi kuendelea kulipa kodi kwa hiari pamoja na matumizi sahihi ya teknolojia na takwimu,” alisema.
Ndejembi alisema mifumo ya kodi inapaswa kutumia teknolojia kurahisisha ulipaji wa kodi kwa hiari, kuboresha huduma kwa walipa kodi na kuwezesha mamlaka za mapato kutumia data katika kufanya maamuzi na kutambua maeneo yenye changamoto.
Alisema mfumo mzuri wa kodi unapaswa pia kuwezesha biashara halali, kuhimiza uwekezaji na urasimishaji wa shughuli za kiuchumi, bila kuweka vikwazo vinavyoweza kudhoofisha shughuli zenye tija.
Akirejea kaulimbiu ya mkutano huo, “Leveraging Technology for Efficient Revenue Collection”, Ndejembi alisema teknolojia inapaswa kusaidia Serikali kupunguza gharama za kiutawala, kurahisisha ulipaji kodi na kuimarisha mazingira ya biashara.
Alisema ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya kodi ni muhimu katika kubadilishana taarifa, uzoefu na mbinu bora za usimamizi wa mapato, huku nchi zikihitaji kutafsiri uzoefu huo katika maboresho yanayoweza kupimika ndani ya mifumo yao.
Ndejembi alisema Tanzania imeendelea kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya kodi, ikiwemo kubadilishana taarifa za kikodi na kutoa usaidizi wa kiutawala kati ya nchi.
Alisema maendeleo hayo yanapaswa kwenda sambamba na kuendelea kuboresha sheria na uwezo wa taasisi ili kuendana na viwango vya kimataifa vya uwazi na usimamizi wa kodi vinavyoendelea kubadilika.
Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Wasimamizi wa Kodi wa Jumuiya ya Madola (CATA), Dkt. Abu Tariq Jamaluddin, alisema jumuiya hiyo inalenga kuwaunganisha viongozi na wataalamu wa kodi ili kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu zinazoweza kuboresha utawala wa kodi.
Alisema katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, CATA imeendelea kuimarisha programu zake katika maeneo ya uongozi, mipango na teknolojia, pamoja na kutumia mijadala ya mtandaoni kuongeza fursa za kujifunza kwa wanachama.
Jamaluddin alisema lengo ni kuboresha utawala wa kodi, kurahisisha ulipaji wa kodi kwa hiari, kuongeza ufanisi wa watendaji na kuimarisha matumizi ya data katika usimamizi wa mapato.
Awali, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), CPA Yusuph Mwenda, alisema Serikali imeendelea kuwekeza katika mifumo ya kisasa ya ukusanyaji na usimamizi wa mapato.

Mwenda alitaja Mfumo Jumuishi wa Usimamizi wa Mapato ya Ndani (IDRAS) kuwa miongoni mwa mifumo hiyo, ukiwa na jumla ya moduli 17 zinazolenga kuboresha utoaji wa huduma na usimamizi wa mapato.
Alisema mojawapo ya moduli hizo inahusu utoaji wa ankara za kielektroniki, inayowawezesha walipa kodi kutoa ankara za kielektroniki kupitia mfumo huo bila kulazimika kutumia mashine halisi.
Mkutano huo unawakutanisha zaidi ya wataalamu na viongozi 400 kutoka nchi 48 za Jumuiya ya Madola kwa ajili ya kubadilishana maarifa na uzoefu kuhusu matumizi ya teknolojia katika kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa kodi.
Mjadala wa mkutano huo pia umejikita katika umuhimu wa kubadili mtazamo wa wananchi kuhusu ulipaji kodi, kuunganisha huduma za kikodi na mitandao ya simu, pamoja na kuweka motisha zitakazohamasisha wananchi kudai risiti wanapofanya malipo.

Leave a comment