
Na Neema Maligana
Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupitia Kituo cha Taifa cha Kudhibiti Matukio ya Sumu (NPCC), imewataka wananchi kuacha kutumia vijiwe kama njia ya kutibu madhara yatokanayo na kung’atwa na nyoka, na badala yake kuwahi katika vituo vya afya au hospitali kwa ajili ya kupata matibabu sahihi kwa wakati.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Kituo cha Taifa cha Kudhibiti Matukio ya Sumu, Yohana Goshashy, wakati akitoa elimu kwa wananchi wa Kibaha, mkoani Pwani, kuhusu namna ya kujikinga na matukio ya kung’atwa na nyoka, hatua zinazopaswa kuchukuliwa endapo mtu atang’atwa na nyoka na madhara yanayoweza kujitokeza iwapo mhanga hatapata huduma ya kitabibu kwa wakati.
Goshashy alisema bado kuna baadhi ya wananchi wanaoamini matumizi ya vijiwe kama tiba ya kuondoa sumu baada ya kung’atwa na nyoka, hali ambayo inaweza kuchelewesha upatikanaji wa huduma stahiki.
“Tunawasihi wananchi kuacha kutumia vijiwe kama dawa ya kutibu mtu aliyeng’atwa na nyoka,” alisema Goshashy.
Alisema mtu anapong’atwa na nyoka anapaswa kuchukuliwa kama mgonjwa anayehitaji huduma ya kitabibu na kupelekwa hospitalini haraka iwezekanavyo, badala ya kutumia tiba ambazo hazijathibitishwa kitaalamu.
Aliongeza kuwa kuwahi hospitalini ni muhimu kwa kuwa wataalamu wa afya wanaweza kufanya tathmini ya hali ya mgonjwa na kutoa huduma kulingana na madhara yaliyosababishwa na kung’atwa na nyoka.
Aidha, aliwataka wananchi kuepuka kutumia njia za kienyeji ambazo zinaweza kuongeza madhara kwa mhanga, ikiwemo kuchanja sehemu iliyong’atwa, kunyonya damu au sumu, kuchoma eneo lililong’atwa au kufunga kiungo kwa nguvu bila ushauri wa kitaalamu.
Goshashy alisema matukio ya kung’atwa na nyoka yanaweza kutokea katika maeneo mbalimbali, hususan ambako shughuli za wananchi zinahusisha kilimo, ufugaji, uwindaji au shughuli nyingine zinazowaweka katika mazingira yenye uwezekano wa kukutana na nyoka.
Mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Soga, Iddi Pasi, alisema katika baadhi ya matukio watu wanapopatwa na changamoto hiyo huanza kutafuta msaada kutoka kwa watu wanaodai kuwa wana uwezo wa kutibu madhara ya sumu kwa kutumia tiba za jadi, hali inayoweza kuchelewesha upatikanaji wa huduma ya kitabibu.

“Changamoto kubwa kwetu ni pale mtu anapong’atwa na nyoka. Mara nyingi watu wanakuwa na hofu na hawajui waanzie wapi,” alisema Pasi.
Alisema wakati mwingine waathirika hupelekwa kwa watu wanaodai kutumia vijiwe au dawa za kienyeji, lakini elimu waliyopewa imewasaidia kuelewa kuwa hatua ya kwanza ni kumfikisha mhanga hospitalini.
Wananchi walioshiriki mafunzo hayo walisema elimu iliyotolewa na Mamlaka itawasaidia kujikinga na nyoka na kuchukua hatua sahihi endapo mtu atang’atwa, huku wakibainisha kuwa changamoto kubwa ni umbali wa vituo vya afya, hofu na ukosefu wa uelewa wa namna ya kutoa msaada wa awali kwa waathirika.

Wananchi wa Boko Mnemela wakimsikiliza mwezeshaji (hayupo pichani), akitoa elimu kuhusu matukio ya nyoka.
Leave a comment